Habari Mseto

Vilio vyashamiri kuhusu gharama ya stima nchini

February 19th, 2024 1 min read

NA BRIAN AMBANI

“WAKATI kama huu mwaka jana, nilikuwa nikinunua vipimo 51 za stima kwa Sh1,000. Sasa napata chini ya 35 kwa kiasi sawa,” analalamika Catherine Wanjiru, mkazi wa eneo la Kasarani Nairobi.

‘Inaniathiri,’ anasema kuhusu kupanda kwa bei ya umeme.

Bi Wanjiru hayuko peke yake.

Mamilioni ya watu na wafanyabiashara wanajipata katika hali sawa huku bei ya umeme ikipanda sana katika mwaka uliopita, na hivyo kupandisha gharama ya maisha na ya kufanya biashara.

Mteja aliyekuwa akilipa Sh20 Februari mwaka jana, kwa wakati huu analipa Sh23 likiwa ongezeko la asilimia 15 katika muda wa miezi 12 pekee.

Watengenezaji, ambao ndio watumiaji wakubwa wa umeme nchini, wanasema gharama ya kuendesha kampuni imepanda kutokana na kupanda kwa bei ya umeme katika miaka ya hivi karibuni.

Muungano wa Watengenezaji bidhaa wa Kenya (KAM), unasema gharama ya kawi imepanda kwa asilimia 59 katika miaka mitatu iliyopita pekee kutoka wastani wa Sh15.8 kwa kipimo Januari 2021 hadi Sh25.1 Januari 2024.

KAM inasema kutokana na hali hiyo, Kenya inapoteza nafasi yake kama kivutio cha uwekezaji katika ukanda huu huku wawekezaji wakimiminika katika nchi jirani hasa Tanzania, Uganda na Ethiopia.

‘Uchumi unafufuka kutoka katika hali tatu ngumu (Covid-19, migogoro ya kimataifa na Uchaguzi Mkuu wa 2022). Ni wakati wa kuunga mkono kila juhudi ili kurekebisha ukuaji wa uchumi. Ongezeko la gharama halina faida,” alisema Mtendaji Mkuu wa KAM Anthony Mwangi.