Habari

Vilipuzi hatari vyapatikana vimefichwa shambani Kitale

May 25th, 2020 1 min read

NA GERALD BWISA

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Trans-Nzoia wametegua vilipuzi vilivyokuwa vimefichwa katika shamba moja eneo la Kitale.

Kilipuzi aina ya M257 FRG na kingine aina ya Yugoslovia M60 kiliteguliwa na mtaalamu wa bomu kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai, afisi ya Kakamega kabla ya kuondolewa kwa shamba hilo.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Trans-Nzoia, Bw Ayub Ali alisema kuwa shughuli nzima iliendeshwa saa sita mchana Jumatatu huku ikihusisha maafisa wa usalama wa kaunti hiyo.

Vilipuzi hivyo viliripotiwa na Bw Dennis Mbugua, meneja wa shamba la Crescent Springs Ltd ambaye alipiga ripoti kwa polisi.

Alisema kwamba aligundua vilipuzi hivyo alipokuwa akichimba shambani kwa trakta baada ya gunia lenye vilipuzi kufukuliwa ardhini kutokana na shughuli za kuchimba.

“Maafisa wetu walipotembelea eneo lenyewe walipata bomu aina ya HE, bunduki aina ya FRG na risasi za kipekee 259 zikiwa zimefungwa ndani ya gunia,” Bw Ali aliambia Taifa Leo.

Alisema kwamba hakuna tukio lililoripitiwa wakati wa zoezi hilo.

“Vilipuzi hivi vinaonekana kuwa zilifukiwa kwa muda mrefu na labda mwenye kufanya hivyo akasahau alipozifukia. Tunafanya uchunguzi wa kisa hiki haraka iwezekanayo.”

Ugunduzi wa vilipuzi hivyo unafuatia kuokolewa kwa bunduki mbili aina ya SHE na G3 pamoja na risasi zilizoibiwa kutoka kwa afisi za Huduma za Misitu huko Saboti wiki chache zilizopita.

Mshukiwa mmoja aliuawa na mwingine kukamatwa kufuatia wizi huo.

Tafsiri: Faustine Ngila