Michezo

Villa wamtwaa fowadi Traore kutoka Lyon

September 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ASTON Villa wamemsajili fowadi Bertrand Traore kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa kwa kima cha Sh2.4 bilioni.

Traore, 25, anarudi kusakata soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuhudumu nchini Ufaransa kwa misimu mitatu.

Nyota huyo raia wa Burkina Faso aliwahi kuvalia jezi za Chelsea kwa miaka mitatu. Anaungana sasa na aliyekuwa mwanasoka mwenzake ugani Stamford Bridge, John Terry ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi uwanjani Villa Park.

“Tuna furaha tele kwamba Bertrand ameteua kuja Villa. Ni mwanasoka anayejivunia utajiri mkubwa wa kipaji ambaye analeta nguvu mpya na msisimko zaidi kwenye safu yetu ya ushambuliaji,” akasema kocha wa Villa, Dean Smith.

Traore ni mchezaji wan ne kuingia katika sajili rasmi ya Villa muhula huu baada ya kikosi hicho kujinasia pia huduma za kipa Emiliano Martinez kutoka Arsenal, Ollie Watkins kutoka Brentford na beki wa kulia, Matty Cash aliyeagana na Nottingham Forest.

Villa wametumia kima cha Sh11.6 bilioni kujisuka upya hadi kufikia sasa muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO