Afya na Jamii

VillageReach yateua Nairobi kitovu cha shughuli zake barani

January 31st, 2024 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

SHIRIKA la huduma za afya la VillageReach limefungua kitovu chake jijini Nairobi kufuatilia kwa ukaribu shughuli zake barani Afrika.

Hii itawezesha shirika hili kukagua kwa ukaribu zaidi shughuli zake katika mataifa ambako linahudumu, vile vile kuunda uhusiano thabiti na washirika wake barani.

Hatua hii aidha, inatoa fursa kwa shirika hili kushirikiana na Wizara ya Afya.

Kama sehemu ya Ruwaza ya 2030 ya shirika hilo, kitovu hiki kitarahisisha ushirikiano kati ya shirika hili na serikali, sekta za kibinafsi na washirika, hapa nchini na kimataifa, ili kunakili na kupima suluhu za huduma ya afya ambazo zinaweza kustahimili matatizo katika utoaji huduma za kiafya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mnamo Jumatano, Afisa Mkuu Mtendaji wa VillageReach Emily Bancroft alisema kwamba kitovu hiki kitaongeza ushirikiano na kuimarisha shughuli katika mataifa 15 ambamo shirika hili linahudumu.

“Huku asilimia 73 ya wafanyakazi wetu duniani wakitekeleza shughuli zao katika maeneo mbalimbali barani Afrika, kituo hiki kitahakikisha kwamba shirika la VillageReach limejiandaa kutimiza  ruwaza yetu mpya mwaka wa 2030,” alieleza Bi Bancroft.

Kulingana na Naibu Mkuu wa Ushirika na Matokeo katika VillageReach Claudia Shilumani, Kenya ilichaguliwa kama kitovu cha shughuli za shirika hilo kutokana na kuwa tayari imeafikia mengi katika sekta ya afya ikilinganishwa na mataifa mengine barani.

Tayari shirika la VillageReach lina ushirkiano wa karibu na Wizara ya Afya katika masuala ya upanuzi na ufikiaji wa huduma za dharura za simu.

Ushirikiano huu unahusisha namna ya kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya kupooza (polio), ambapo shirika hili limehusika katika kuimarisha shughuli za usafirishaji wa sampuli, vile vile kuhakikisha kwamba zinawasilishwa kwa ubora wa hali ya juu, kutoka vituo vya afya vya kijamii, hadi katika maabara ya kitaifa na kimataifa.

Shirika la VillageReach aidha linashirikiana na Wizara ya Afya katika Kaunti ya Migori, kuhakikisha kwamba wahudumu wa afya wa kijamii wanapata vifaa vya afya, kando na kushirikiana na sekta ya kibinafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kusaidia Wizara ya Afya kuunda sera za kiafya kupitia data.

Shirika la VillageReach lilianzia shughuli zake nchini Msumbuji miaka 23 iliyopita, na kwa sasa linashirikiana na serikali, sekta za kibinafsi na washirika wa kiufundi katika mataifa 15 barani Afrika.

[email protected]