Kocha Unai Emery aongoza Villarreal kupiga Young Boys kwenye UEFA baada ya kukataa ofa ya kunoa Newcastle

Kocha Unai Emery aongoza Villarreal kupiga Young Boys kwenye UEFA baada ya kukataa ofa ya kunoa Newcastle

Na MASHIRIKA

UNAI Emery, 50, aliongoza Villarreal kutandika Young Boys 2-0 kwenye mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku, saa chache baada ya kutupilia mbali ofa ya kuwa kocha mpya wa Newacastle United.

Emery ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG), Sevilla na Arsenal, alikuwa akipigiwa upatu wa kuwa mrithi wa kocha Steve Bruce kambini mwa Newcastle ambao sasa wanamilikiwa na mabwanyenye kutoka Saudi Arabia.

Awali, ilitarajiwa kwamba mechi dhidi ya Young Boys ingalikuwa ya mwisho kwa Emery ambaye ni raia wa Uhispania kusimamia kambini mwa Villarreal ambao sasa wamejizolea alama saba sawa na viongozi wa Kundi F kwenye UEFA, Manchester United.

Chini ya Emery, Villarreal walitawazwa wafalme wa Europa League mnamo Mei 2021 baada ya kuwazamisha Man-United kupitia mikwaju ya penalti. Kufikia sasa, wameshinda mechi mbili kati ya nne kwenye kampeni za UEFA muhula huu.

Wakicheza dhidi ya Young Boys, Villarreal waliweka kifua mbele na Etienne Capoue kabla ya bao la Christian Fassnacht wa Young Boys kufutiliwa mbali kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Fowadi wa zamani wa Bournemouth, Arnaut Danjuma alifanya mambo kuwa 2-0 mwishoni mwa kipindi cha pili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa maharagwe

SHINA LA UHAI: Kansa ya matiti: Wanaume msiipuze!

T L