Dondoo

Vimada wafyonza jasho la paparazzi

July 20th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

VOI MJINI

Jamaa aliyekuwa paparazzi maarufu mjini humu anajuta kuuza simu na kamera yake kwa bei ya kutupa ili apate pesa za kufurahisha vimada wake!

Kulingana na duru zetu, kalameni huyo alikuwa ameokoka hapo awali na kuwa kielelezo chema katika jamii. Wakati huo alienziwa na kila mtu mtaani kutokana na upole wake na tabia yake.

“Polo alikuwa ndugu katika Yesu hapo awali na pia mzee wa kanisa. Alikuwa mfano mzuri wa kuigwa janibu hizi,” alisema mdaku wetu.

Hata hivyo, wokovu wake haukudumu kwa muda mrefu, aliingilia ulevi na kuwaacha wengi vinywa wazi.

Inasemekana kila alipopata pesa kutokana na kazi yake ya kupiga picha katika sherehe na hafla za kijamii, alikuwa akifululiza moja kwa moja hadi kwa mama pima kupata dozi na pia kuwafurahisha wanawake.

“Polo aliibuka kuwa mraibu sugu wa pombe na mbadhirifu mkubwa. Pesa zote alizokuwa akichuma zilikuwa zinaishia ulevini,” alisema mdokezi wetu.

Inaarifiwa kuwa, kwa sababu ya janga la corona, kazi ya kupiga picha iliadimika maana sherehe zilipigwa marufuku na polo akakosa njia za kujipatia riziki na pia kutuliza kiu yake.

Ripoti za mtaa zaarifu kuwa, alipowaza na kuwazua, aliamua kuuza simu na kamera yake kwa bei duni ili apate hela za kuburudika na vimada wake kwa mama pima.

Inasemekana kwa sasa polo hana mbele wala nyuma. “Anahangaika mjini hapa akijuta kuuza vifaa vyake vya kazi. Ni kweli cha mlevi huliwa na mgema na majuto ni mjukuu, huja baadaye,” asema mdokezi.