COVID-19: Vinara wa EPL wahimiza wachezaji kuchanjwa

COVID-19: Vinara wa EPL wahimiza wachezaji kuchanjwa

Na MASHIRIKA

VINARA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Serikali ya Uingereza wamehimiza wanasoka kuchanjwa dhidi ya Covid-19.

Nusu ya mechi za EPL zilizokuwa zitandazwe wikendi hii tayari zimeahirishwa kutokana na ongezeko la maambukizi ya corona linalozidi kushuhudiwa katika klabu mbalimbali.

Katika ligi za daraja za pili, tatu na nne nchini Uingereza (EFL), asilimia 25 ya wachezaji tayari wamesema hawana nia ya kuchanjwa na tayari mechi 19 zilizokuwa zitandazwe Jumamosi ya Disemba 18, 2021 zimeahirishwa.

Kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp wa Liverpool, hatua ya wanasoka kuchanjwa ni dhihirisho la kiwango cha juu cha uwajibikaji. Mkufunzi huyo raia wa Ujerumani amefichua kwamba asilimia 99 ya kikosi chake kimepokea dozi mbili za chanjo.

Maoni sawa na yake yanashikiliwa pia na makocha Mikel Arteta na Pep Guardiola wa Manchester City.

Hali ilivyo katika Ligi Kuu za bara Ulaya:

Italia

  • Serie A inasema asilimia 98 ya wachezaji wa kipute hicho imepokea dozi mbili za chanjo. Beki wa Juventus na Italia, Giorgio Chiellini alitumia mtandao wa kijamii mwanzoni mwa Disemba kuhimiza wachezaji wenzake kupokea chanjo.

Ufaransa

  • Asilimia 95 ya wachezaji wamepokea dozi mbili za chanjo na visa vichache sana vya maambukizi mapya vimeripotiwa katika Ligue 1.

Ujerumani

  • Asilimia 94 ya wachezaji wamepokea dozi mbili za chanjo. Beki Joshua Kimmich wa Bayern Munich alipatikana na virusi mnamo Novemba na akajuta maamuzi yake ya kutochanjwa mapema.

Uhispania

  • Zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wamepokea dozi mbili za chanjo na klabu ziko huru kujaza mashabiki viwanjani wakati wa mechi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

STAA WA SPOTI: Malkia wa tenisi anayeikweza Kenya Afrika na...

NYOTA WA WIKI: Karim Benzema

T L