Vinara wa OKA sasa waalikwa kwa ndoa ya Uhuru na Raila

Vinara wa OKA sasa waalikwa kwa ndoa ya Uhuru na Raila

Na BENSON MATHEKA

Vigogo wa kisiasa wanaounga handisheki, wamealikwa katika muungano wa kisiasa unaosukwa kati ya vyama vya Jubilee na ODM.

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju anasema kwamba muungano huo unaosukwa kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga hautawafungia vinara wa vyama vingine vinavyotaka kuungana nao.

Hata hivyo, alisema watakubali tu vyama ambavyo havitawapatia masharti. Vyama vya Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka na Kanu cha seneta wa Baringo Gideon Moi vina mkataba wa ushirikiano na Jubilee.

Imeibuka kwamba hatua ya ODM kuungana na Jubilee iliudhi washirika wa Bw Odinga katika muungano wa NASA ambao walitegemea kuidhinishwa na Rais Kenyatta kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Musyoka na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, wameapa kwamba hawatamuunga Bw Odinga kugombea urais.

Kulingana na Bw Tuju, Jubilee na ODM vimekuwa vikishirikiana ndani na nje ya bunge na vinaandaa mikakati kubuni muungano.

“Sisi, katika mrengo wa Jubilee tunafanya mazungumzo na ODM tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kwa minajili ya kuunda muungano,” Tuju akasema.

Alitangaza Ijumaa kuwa kamati imeundwa, ili kuandaa mikakati ya kubuni muungano.

Tuju alisema kamati hiyo itatoa ripoti chini ya siku 14, na kwamba vyama vingine vya kisiasa vinakaribishwa kujiunga na muungano utakaobuniwa.

“Sio muungano wa kushurutishwa,” alisema. Hata hivyo, duru zinasema kwamba Rais Kenyatta amekuwa akiwarai vinara wenza kwa NASA kuungana nyuma ya Bw Odinga ili kumshinda Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hatua ya Jubilee kuhalalisha ushirikiano wake na ODM inaashiria kwamba huenda Rais Kenyatta atamchagua Bw Odinga kuwa mrithi wake.

Kalonzo na Raila nao wamekuwa wakitofautiana hadharani kuhusu safari ya kuelekea Ikulu 2022.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV, Kalonzo alinukuliwa akisema atakuwa mtu mjinga duniani kuunga mkono Bw Raila Odinga 2022 kuwania urais kwa mara ya tatu.

“Kwa sasa, hata haiwezi ikafirika, mimi Kalonzo Musyoka, nitamuunga Raila Odinga mara ya tatu. Nitakuwa mtu mjinga duniani kumuunga mkono mara ya tatu bila ya yeye kurudisha mkono,” akasema.

Kiongozi huyo wa Wiper alilaumu chama cha ODM kwa kile alitaja kama “usaliti” na kusambaratisha NASA, muungano ambao ulileta pamoja Bw Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetangula (Ford Kenya) kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Mnamo Alhamisi akiwa Mombasa, Bw Odinga alisema hajamuomba yeyote kumuunga mkono na kwamba hajatangaza azima yake ya kuwania urais.

“Sijatangaza mimi nataka kusimama urais, lakini wengine wanasema eti hawawezi kuniunga mkono, nimekuuliza wewe uniunge mkono? Mimi sijatangaza, sasa wewe unaanza kutetemeka, unaanza kubwekabweka, subiri bwana mambo bado,” alisema.

Hata hivyo, muungano unaosukwa kati ya chama chake na Jubilee unaonyesha kuwa atakuwa kwenye debe.

Jana, washirika wa Naibu Rais William Ruto ambao wanaunga chama cha United Democratic Alliance walikejeji muungano wa ODM na Jubilee wakisema ni wa makabila na hauwatishi.

You can share this post!

Nassir na Shahbal walilia ‘tosha’ ya Raila...

Uzinduzi wa chama kipya Mlima Kenya waahirishwa