Habari Mseto

Jinsi ving'ora vilivyochanganya wakazi

February 24th, 2020 1 min read

Na Sammy Kimatu

[email protected]

HOFU ilitanda katika mitaa ya mabanda ya Mukuru-Sinai sawia na Mukuru-Lunga Lunga baada ya sauti kubwa ya ving’ora kusikika kutoka kwa ambulansi, magari ya Msalaba Mwekundu pamoja na ya polisi.

Watu walidhani kulikuwa na moto katika barabara ya Nanyuki ambayo ni eneo la shughuli nyingi kutokana na mafuta kutoka bohari la Nairobi.

Aidha, ni eneo lililo karibu na mtaa wa mabanda wa Mukuru- Sinai ambapo tukio la moto ulioua watu 100 lilitokea mnamo mwaka 2011.

“Lengo letu lilikuwa kufanya mazoezi kupima utayari wa kukabiliana na dharura tukishirikiana na wadau wote,” Bw Wilson Kimondo, Meneja wa kampuni ya Lake Oil Kenya akasema.

Hafla hiyo hufanyika katika kila robo ya mwaka ambapo wakati huu iliandaliwa na Lake Oil Kenya.

Bw Kimondo ameongeza kuwa wakazi wa zoezi hilo, walimwaga mafuta huku timu ya kukabiliana na majanga ya dharura ikiingia.

Kulikuwa na wale wanazima moto, waokoaji na maafisa wa polisi wa kudhibiti eneo la tukio.

Kadhalika, polisi wa trafiki waliongoza magari katika barabara ya Nanyuki, Barbara ya Likoni sawa na barabara ya Lunga Lunga yenye shughuli nyingi.

Barabara zote zimo katika eneo la Viwandani.

Walioshiriki ni pamoja na Kenya Pipeline, Gulf Energy, National Oil, Vivo, Kaunti ya Nairobi, Lake Oil, na Oil Libya.

Wengine walikuwepo ni pamoja na kampuni ya LPG, Huduma ya Polisi ya Kenya, Msalaba Mwekundu wa Kenya, maafisa wa utawala na wawakilishi wa wakazi wa mitaa ya Mukuru hasa Lunga Lunga.

“Tunazunguka kila wakati tunapokuwa na hafla baada ya uteuzi kufanywa, ndipo tutajipanga tukizishirikisha depo zote za mafuta saba, ” Bw Kimondo aliambia Taifa Leo.