Michezo

Vinicius na Benzema waongoza Real Madrid kuzamisha Levante ligini

October 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real Madrid, waliendeleza mwanzo bora katika kampeni za msimu huu kwa kuwafunga wenyeji wao Levante mabao 2-0 mnamo Oktoba 4, 2020.

Fowadi chipukizi raia wa Brazil, Vinicius Junior alifunga bao katika mechi mbili mfululizo za La Liga kwa mara ya kwanza baada ya kukamilisha kwa ustadi mpira wa kona alioelekezewa na kiungo Luka Modric kunako dakika ya 16.

Karim Benzema alifunga bao la pili la Real mwishoni mwa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga baada ya kusajili ushindi katika jumla ya mechi tatu zilizopita mfululizo.

Mbali na kufunga bao, Benzema alishuhudia kombora lake katika kipindi cha pili likigonga mhimili wa goli la Levante huku Vinicius naye akipoteza nafasi nyingi za wazi alizoandaliwa na Benzema na nahodha Sergio Ramos.