Vinono bungeni vyapasua ODM

Vinono bungeni vyapasua ODM

NA ONYANGO K’ONYANGO

UHASAMA mkubwa umeibuka kati ya wanasiasa vijana na wale wakongwe ndani ya ODM kuhusu nyadhifa za uongozi, hali ambayo inatishia kusambaratisha uthabiti wa chama hicho.

Tofauti hizi zimeanza kushamiri baada ya Kinara wa ODM Raila Odinga kulemewa na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. ODM ndiyo chama cha pili chenye wabunge wengi zaidi baada ya UDA anayoiongoza Rais Ruto.

Tangu ODM Ibuniwe mnamo 2005, chama hicho kimekuwa na ufuasi mkubwa hasa katika maeneo ya Nyanza, Magharibi, Pwani na Kaskazini Mashariki. Hata hivyo, baada ya Bw Odinga kushindwa, ODM imeanza kukosa udhabiti huku wabunge wake wakikabiliana mitandaoni kuhusu mamlaka bungeni.

Hapo jana, baadhi ya wabunge vijana waliteta kuwa uongozi wa ODM umekuwa wa kiimla na umewasaliti vijana kwa kuwafungia nje katika nyadhifa za juu za bunge.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wiki jana ilitangaza orodha ya wanasiasa wa kushikilia nyadhifa mbalimbali katika mabunge ya kitaifa na seneti. Orodha hiyo ndiyo imezua uhasama kati ya wabunge wa ODM.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina jana Ijumaa alieleza Taifa Leo kuwa amekuwa akipigania Bw Odinga ila hakuna anayethamini juhudi zake na ODM sasa inasimamiwa kama chama cha watu wa Nyanza na Magharibi pekee.

“Kila mtu anafahamu kile ambacho nimefanyia ODM na ni wakati nastahili kutunuliwa kutokana na juhudi zangu. Karibu nife nikipigania Raila na kama hilo halitoshi kutuzwa basi nielezwe waziwazi,” akasema Bw Ole Kina huku akisisitiza hatakihama chama hicho.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Ijumaa, Mbunge wa Embakasi Mashariki Bw Babu Owino alisema kuwa wale ambao walifanya bidii wakati wa kampeni za Bw Odinga wanastahili kutunukiwa.

Bw Owino alidai kuwa mbunge maalum John Mbadi alitishia kujiuzulu iwapo hangepewa mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC) baada ya kukosa wadhifa wa Kiongozi wa Wengi.

“Wabunge wa Azimio walipendekeza nipewe uenyekiti wa PAC. Hata hivyo, Mbadi alitishia Bw Odinga kuwa angejiuzulu iwapo hangetunukiwa wadhifa wa PAC baada ya nafasi aliyokuwa akiotea kupewa mwengine. Baba aliamua kumpa bila kushauriana nami,” akasema mbunge huyo.

Alimtaka Bw Mbadi amheshimu kwa kuwa alipigania uteuzi wake na kumuunga mkono kama mwenyekiti wa ODM.

Hata hivyo, Bw Mbadi naye alikanusha kuwa alitishia kujiuzulu akisema kuwa kama hakukihama chama baada ya kushurutishwa kuzima azma yake ya ugavana basi hawezi kufanya hivyo saa hii.

“Raila si mtu wa kutishiwa na Babu hastahili kumhusisha na malalamishi yake. Hakuna kipindi nilitishia kujiuzulu kutoka kwa chama. Pia sijasalitiwa na chama. Nimelalamika tu kuwa sijashughulikiwa vizuri kutokana na matarajio yangu,” akasema Bw Mbadi.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero aliwaunga mkono Mabw Owino na Ole Kina, akisema kuwa vijana ndio walitekeleza majukumu muhimu kuvumisha ODM na wanastahili kutuzwa.

“ODM imefika mahali ipo kutokana juhudi za vijana na wanastahili kupokezwa nafasi yao. Inasikitisha kuwa nyadhifa zikigawiwa, wakongwe ndio hunufaika. Hii inaonyesha wazi kuwa ODM ni mali ya mtu binafsi na inatumika kumtajirisha mmiliki,” akasema Bw Kidero.

Mbunge wa Saboti Caleb Amisi naye alidai kuwa wale ambao wanatunikiwa vyeo ndio walisababisha Bw Odinga kupoteza kura za Urais. Hata hivyo, aliwataka wanaolalamika kuandaa mazungumzo na Bw Odinga kuhusu suala hilo.

“Ni kweli wenzetu kutoka mrengo mwingine wanathaminiwa sana. Hata hivyo, hakuna haja ya kutishia uongozi wa chama badala yake tukumbatie maelewano. Vijana wathaminiwe kwa sababu ni hawa wazee ndio walisababisha Bw Odinga ashindwe,” akasema Bw Amisi.

Wabunge Samuel Atandi (Alego Usonga) na Christopher Aseka (Khwisero) hata hivyo walisema tofauti hizo zinaonyesha kuwa ODM ni chama kinachozingatia demokrasia kwa kuruhusu maoni kinzani.

“Wanalalamikia vyeo vya ubunge ambavyo wanadai wanastahili kutunukiwa. Pia wanaamini kuwa wao ni bora kuliko wengine. Siungi mkono kile wanachofanya kwa sababu kiongozi wa chama ashatoa mwelekeo kuhusu suala hilo,” akasema Bw Aseka.

Tofauti hizo zinajiri wakati ambapo Bw Odinga anaonekana kuanza kuishiwa makali kisiasa na wiki jana alilazimika kukita kambi Nyanza kushawishi madiwani wawachague baadhi ya wandani wake kama Maspika. 

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wakati wa serikali mpya kuinusuru soka ni sasa

Hofu Ebola ikichacha Uganda

T L