Vinyago wa Uhuru

Vinyago wa Uhuru

Na WANDERI KAMAU

YAMKINI Rais Uhuru Kenyatta ameonekana kuwateka kisiasa kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka.

Hali hii imeibua maswali ikiwa wawili hao kweli watajibwaga kwenye kinyang’anyiro cha urais utakaofanyika baadaye mwaka ujao au wanatumika kama chambo cha kuvutia kura kwa niaba ya mgombeaji maalumu.

Tangu 2018, baada ya handisheki kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Rais Kenyatta amekuwa akiwashirikisha wawili hao katika baadhi ya mipango ya serikali na mikakati yake ya kisiasa, ingawa uhusiano uliopo baina yao bado haujabainika rasmi.

Kwa mfano, wawili hao walikuwa miongoni mwa vigogo wa kisiasa walioshirikishwa na serikali kwenye mchakato wa uzinduzi wa Huduma Namba mnamo 2019.

Kwenye uzinduzi huo Aprili 1, 2019, Bw Mudavadi aliongoza shughuli hizo katika Kaunti ya Kajiado, huku Bw Musyoka akiongoza uzinduzi huo katika Kaunti ya Murang’a.

Mnamo Julai 2019, Rais Kenyatta alimteua Bw Musyoka kuwa Mjumbe Maalum wa Kenya nchini Sudan Kusini.

Taarifa kutoka kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ilisema, uteuzi wa Bw Musyoka “unalenga kuisaidia taifa hilo kuharakisha mchakato wa kupata amani.”

Tangu uteuzi huo, Bw Musyoka amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara kwenye vikao vya mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo kama mwakilishi rasmi wa Kenya.

Katika hatua iliyoonyesha “kuongezeka kwa ukaribu kati ya Bw Musyoka na Rais Kenyatta”, Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la Wiper lilitangaza kuunga mkono hatua ya chama hicho kubuni ushirikiano wa kisasa na Chama cha Jubilee (JP) Julai mwaka uliopita.

Mpaka sasa, mustakabali wa mkataba huo haujulikani, hasa baada ya Wiper kujiondoa katika muungano wa NASA na kujiunga na ule wa Okoa Kenya Alliance (OKA), unaovishirikisha vyama vya ANC, Ford-Kenya na Kanu.

Upeo wa ‘ukaribu’ wa viongozi hao na Rais Kenyatta ulikuwa ni kushirikishwa kwao kwenye harakati za kuuvumisha Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI), ambao baadaye uliharamishwa na mahakama.

Mabwana Mudavadi na Kalonzo walijumuishwa kwenye kila harakati za kuupigia debe mswada huo, kama mikutano na kampeni zilizofanyika katika sehemu mbalimbali nchini.

Licha ya juhudi hizo, wadadisi wa siasa wanasema, kuna uwezekano Rais Kenyatta anawachezea tu kisiasa, ikizingatiwa licha ya kusisitiza watakuwa debeni 2022, wanaonekana kuendelelea kudhibitiwa na Rais.

“Ni wazi Rais Kenyatta anawachezea tu viongozi hao. Ukosefu wa mwelekeo dhahiri wa kisiasa uliopo baina yao na Rais unaashiria hali tepetevu ambayo huenda ikawaathiri pakubwa ielekeapo 2022,” asema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa siasa.

Mnamo Agosti, Rais Kenyatta alikutana mara mbili na muungano wa OKA, baada ya Mahakama ya Rufaa kuunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu kuharamisha BBI.

Ijumaa, vigogo hao walilazimika kuahirisha mikutano kadhaa waliyokuwa wamepanga kufanya katika Kaunti ya Vihiga, baada ya kuitwa kwa ghafla na Rais Kenyatta.

Kama Bw Musyoka, Bw Mudavadi amekuwa akisisitiza ni lazima awe debeni 2022.

Hata hivyo, wadadisi wanasema hatua yao ya kuahirisha mikutano yao Ijumaa ili “kutii” mwito wa Rais ni ishara wawili hao hawawezi kujisimamia kisiasa, bali wanategemea “uungwaji mkono kutoka nje.”

“Kutapatapa huko kunaonyesha huenda wawili hao hatimaye wakasalimu amri na kutii maagizo ambayo watapewa na Rais Kenyatta. Wangekuwa wanasiasa wanaojiamini, wangeshaanza kuvumisha azma zao kama wanavyofanya Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Vigogo hao wamekuwa wakilalamika kwamba, Rais Kenyatta amekuwa akiwashinikiza kumuunga mkono Bw Odinga kuwania urais 2022, rai wanayosema hawatakubali hata kidogo.

“Hatutakubali kushinikizwa na yeyote kumuunga mkono kiongozi yeyote kuwania urais. Wakenya ndio watafanya maamuzi hayo,” akasema Bw Mudavadi, Jumapili, kwenye kauli aliyoonekana kumwelekezea Rais Kenyatta.

Wadadisi wanasema vigogo hao wako kwenye njiapanda kisiasa, kwani wanahofia kuwa katika baridi ya kisiasa.

“Wawili hao wamekuwa nje ya serikali tangu 2013 baada ya kuhudumu kama Naibu Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mtawalia katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki. Hofu ya kuwa nje ya siasa 2022 ndiyo chanzo cha kutapatapa kwao kisiasa,” asema Bw Mutai.

You can share this post!

Mahakama yaagiza Rotich ashtakiwe upya

Nafuu kuu watalii wakifurika Mombasa

T L