Habari Mseto

Vioja mkuu wa hospitali akijifungia ofisini asipewe barua ya kufutwa

December 14th, 2018 1 min read

Na Walter Menya

HALI ya taharuki iliibuka katika Nairobi Hospital Ijumaa, wakati bodi ya wasimamizi ya hospitali hiyo ilijaribu kumtimua Afisa wake Mkuu Mtendaji (CEO) Gordon Odundo.

Vioja vilianza wakati wakili wa bodi hiyo alimpelekea barua ya kufutwa kazi Bw Odundo, ambapo afisa huyo anasemekana kujifungia katika ofisi yake ili asipokezwe barua.

Wakili huyo naye ambaye alikuwa ameandamana na afisa wa usalama alilazimika kupiga kambi nje ya ofisi ya mkuu huyo wa hospitali hadi saa nane alasiri.

Hatua hiyo ilikuja siku moja tu baada ya aliyekuwa Rais Daniel Moi kulazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.

Rais huyo mustaafu amekuwa akipokea matibabu ya kuimarisha afya yake ndani na nje ya nchi na sasa anaripotiwa kuwa atalazwa kwa siku nne ili ahudumiwe na madaktari ipasavyo.

Afisa huyo alichukua wadhifa huo chini ya mwaka mmoja uliopita na kumekuwa na manunguniko kuwa huduma imedorora.