Makala

Viongozi kadha wasema raia wanathubutu 'kuwaua ndugu wangali hai'

February 22nd, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

NIA ya Wakenya wanaotumia ujanja kufikia hatua ya kudanganya kuwa fulani amefariki, ni kurina asali ya pesa kutoka kwa viongozi.

Viongozi wengi hapa nchini wamelia kuwa hutapeliwa vitita vikubwa vya pesa na Wakenya ambao hufeki maombolezi, mazishi, magonjwa na harambee za kila aina.

Katika njama hiyo ambayo imeshika kasi katika maeneo mengi ya hapa nchini, kuna baadhi hata hualika marafiki katika harambee za kuchanga pesa za kuwasafirisha wapendwa wao hadi ng’ambo kwa matibabu spesheli, pesa zinachangwa lakini wanaishia kuwalaza wapendwa hao wao katika hospitali za hapa nchini na kuishia kujivinjari na michango hiyo.

Wengine wanaripotiwa kuwa huunda akaunti za benki na za mitandao ya simu na kulipia matangazo ya kibiashara katika vyombo vya habari wakirai Wakenya wasaidie kuokoa maisha au kushirikisha mazishi lakini nyingi ikiwa tu ni miradi ya kuunda vya haramu kupitia hisia za majonzi.

Pia, wafanyakazi walio na udhaifu wa ulevi kiholela wakati wamejipata wamekosa kufika kazini wanaripotiwa kuwa baadhi yao hughushi hali za misiba na magonjwa ili kujipa likizo ya kwendelea kulewa na pia wakibahatika kupokezwa usaidizi wa kifedha na wafanyakazi wenzao kama kitulizo cha dhiki.

Viongozi wengi, wengine wakiomba wasitajwe ili wasijipate wameorodheshwa kama ‘mkono gamu’ na wapiga kura wao wanakiri kuwa hata ikiwa wengi wa walio katika nyadhifa za uongozi hushutumiwa kuwa ni mafisadi ambao hughushi safari, mikutano na ziara za kikazi ili kuvuna marupurupu haramu, hata Wakenya wa kawaida huwa ndiyo hatari zaidi katika njama hizo.

“Ukijua vile sisi kama wanasiasa hukamwa kama ng’ombe bila huruma na tunaowakilisha katika siasa, ungetuelewa wakati tunadai tuongezewe mishahara. Lakini kwa kuwa hakuna anayetaka kuchunguza kuhusu kashfa hii ya sisi kutapeliwa na wapiga kura, tunabaki tu tukiumia bila mtetezi,” alia mbunge wa Suba Kaskazini, Millie Odhiambo.

Mbunge afichua

Mbunge huyo ameamua kupasua mbarika kuhusu vile amekuwa akijipata katika mtego huo wa kuvunwa vya haramu, na akifahamu kuwa kuna hatari ya wapiga kura kumworodhesha kama asiyewajali wakati wa dhiki, hujipata tu anatuma pesa.

“Mimi husimama na wapigakura wangu nyakati za faraja na za dhiki. Eneobunge langu limekuwa likikumbwa na ongezeko la mazishi na ambapo kila Alhamisi na Ijumaa, huwa nimealikwa kusaidia familia kadhaa. Kwa kuwa haiwezekani niwe katika mazishi hayo yote kwa wakati mmoja, huwa ninatuma wasaidizi wangu wakaniwakilishe huku kwingine nikituma mchango wangu kupitia huduma  za simu,” asema Bi Odhiambo.

Ajabu ni kwamba, hata hawa viongozi pia huchezeana ngware ya hadaa za aina hii ambapo baadhi yao pia huchangisha pesa kutoka kwa wenzao ili kusaidia harambee na miradi ya kimaendeleo ambayo ni hewa tu.

“Kuna mbunge wa Kaunti ndogo ya Maragua ambaye kati ya 2004 na 2007 alitutapeli wakati alitutangazia kuwa alikuwa amepata shirika moja la Marekani ambalo lilikuwa limejitolea kufadhili masomo ya juu kwa walimu 10,000 wa hapa nchini. Alituambia kuwa usajili wa mwalimu mmoja ulikuwa ugharimu Sh50,000. Wengi wetu tuliteua walimu kutoka maeneo yetu na tukawalipia usajili huo. Hadi leo hii, hatujarejeshewa pesa zetu, na bado tulioteua wasafiri hadi marekani wangali wanangoja watangaziwe siku na saa ya kuabiri  ndege,” asema.

Hata hivyo, Bi Odhiambo anasema kuwa amekuwa akihoji jinsi mialiko hiyo ya kusaidia mazishi imekuwa ikiongezeka na akaamua kuchunguza.

“Nimekuja kutamnbua kuwa wengi wa Wakenya huwadanganya viongozi wao sio kwa kupenda, bali kwa kuwa ni masikini na wangetaka kuhakikishia familia zao chakula. Kati ya mazishi kumi ambayo nilialikwa wiki jana, nilitambua mawili yalikuwa feki,” asema.

Anasema kuwa wale ambao wanajuana moja kwa moja na viongozi ndio hatari kuu katika biashara hiyo ya kughushi misiba ili wachangiwe.

“Lakini hakuna kile ninaweza nikafanya. Siwezi nikawashutumu wapiga kura wangu ili wakome tabia hiyo…Lakini katika uongozi ni lazima ujiandae kutapeliwa,” asema.

Lakini ukifikiria viongozi ndio tu hutapeliwa katika njama hizi, wakenya wa kawaida pia hujipata wameandaliwa njama ya kugeuzwa kuwa mradi wa pato haramu kupitia maombolezi feki.

Katika mtaa wa Park Road Jijini Nairobi, mwishoni mwa mwaka jana vijana ambao hufanya kazi katika karakana za magari walipata ujumbe kuwa mmoja wao alikuwa amepoteza mamake mzazi.

“Kwa kawaida, huwa tunapigana jeki ya kimaisha na tulipanga kuwa ni lazima tungekutana na tuunde kamati ya kusaidia mwenzetu ambaye ni mzaliwa wa eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu. Tulichanga jumla ya Sh45,000 na tukamkabidhi mwenzetu ambaye alisema angesafiri mapema ili akashirikishe maandalizi ya mazishi nyumbani kwao,” asema Gregory Mwiti, katibu wa muungano wa vijana hao wa karakana eneo hilo.

Anasema kuwa siku ya mazishi waliungana pamoja na wakateua watu 14 wa kwenda kuwakilisha muungano huo katika mazishi.

“Nilikuwa mmoja wa hao 14. Kufika Githunguri katika kijiji cha Kagwi, yule mama tulikumbana naye tukimuomba atuelekeze kwa mazishi hayo alikuwa ni mamake mzazi mwenzetu. Yule tuyliyekuwa tumejitokeza kusindikiza akienda zake kuzimu, alikuwa ndiye huyu akiwa hai na tukimuulizia njia ya kufika kwa mazishi yake,” asikitika.

Mwekezaji katika sekta ya elimu na mikahawa, Lizzie Wanyoike anasema kuwa amekuwa akijipata katika mtego huo.

“Sio mara moja nimepata ujumbe kutoka wengi wa tunaojuana wakinifahamisha kuhusu aidha harambee ya kuchanga pesa za bili za hospitali, za kutoa mwili kutoka mochari ya mbali na kwao, kufadhili mazishi au hata kugharamia usafiri wa familia hadi mochari. Kuna wakati nimejitolea kufika mwenyewe na sio mara moja nimejipata kuwa hakukuwa na msiba wowote bali ilikuwa tu ni njama ya kuunda kidogo ya unga,” asema Bi Wanyoike.

Kisa ambacho kilikuwa na ubunifu zaidi kinaripotiwa na Kamishna wa Narok, George Natembeya ambaye anasema mwaka wa 2016 akihudumu Kaunti ya Isiolo, alipata ujumbe kutoka askari wake mmoja wa kuarifu kuwa alikuwa mgonjwa na hangeweza kufika kazini.

“Askari huyo hakujua kuwa tayari nilikuwa na ripoti kuhusu alikokuwa akilewa pombe. Alitaka nimtumie Sh5,000 za kugharamia familia yake na matibabu pia, akisema alikuwa amevunjika mguu katika ajali ya bodaboda,” asema.

Natembeya anasema kuwa alituma maafisa wengine wawili hadi katika mtaa ambao askari huyo alikuwa akilewa pombe ili wakamkamate.

“Lakini kuna undugu katika njama hizi. Wale askari niliowatuma walishirikiana na mwenzao, wakampeleka hospitalini na akawekwa plasta katika mguu ambao haukuwa umevunjika. Aliletwa afisini akiwa anachechemea katika uigizaji murwa wa maumivu. Nilitazama tu kwa umbali, nikajua ‘nimepigwa Kiswahili’. Nilijiunga na maafisa wenzangu kuchangia jamaa huyo,” asema.

Ni katika hali hiyo ambapo aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau anapendekeza kuwa serikali itwae kazi za kugharamia bili za magonjwa na mazishi kwa wote ambao watasajiliwa kuwa masikini hohehahe.

Mbau anasema kuwa atashinikiza serikali kupitia mswada wa kibinafsi bungeni itenge Sh20bn kila mwaka za kugharamia mazishi na bili za hospitali za wananchi maskini.

Anapendekeza kuwa serikali iwe ikitoa Sh50,000 kwa kila maskini hohehahe ambaye ana matanga na pia matibabu ya bure kwa wote ambao hawajiwezi kimaisha.

“Hatua hii itaishirikisha idara ya utawala wa Mikoa ambapo machifu na manaibu wao watakuwa na jukumu la kuwatambua masikini katika maeneo yao. Hali hii itazima ubunifu wa matanga na magonjwa kutumiwa kama mradi wa kuunda pesa,” akasema.