Viongozi kadhaa Kiambu wajiunga na UDA

Viongozi kadhaa Kiambu wajiunga na UDA

Na LAWRENCE ONGARO

UHASAMA wa kisiasa kati ya viongozi wawili Kaunti ya Kiambu unazidi kutokota.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina, na aliyekuwa gavana wa Kiambu hapo awali Ferdinand Waititu, wanalenga kuwania kiti cha ugavana cha Kiambu.

Wengine ambao pia wamo mbioni kutegea kiti hicho ni gavana wa sasa Dkt James Nyoro na Seneta Kimani Wamatangi.

Mwingine ni Bw William Kabogo aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo ambaye yumo mbioni kukipa umaarufu chama chake cha Tujibebe Wakenya Party.

Siasa za Kaunti ya Kiambu zinazidi kuwa na ushindani mkali huku kizungumkuti kikiwa ni chama cha kutafuta uongozi kupitia kwacho.

Naibu Rais Dkt William Ruto alipozuru Kaunti ya Kiambu, viongozi kadha wa Mlima Kenya wakijitokeza kumkaribisha.

Baadhi yao ni mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina, Ferdinand Waititu, na Alice Ng’ang’ a aliyekuwa mbunge wa Thika hapo awali.

Sasa kizungumkuti cha kisiasa ni kati ya Wainaina na Waititu ambao wote wamejitambulisha na chama cha UDA.

Hata tayari Bw Wainaina alivishwa kofia ya manjano mbele wa umati ili kuthibitisha ufuasi wake kwa Dkt Ruto.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina, PICHA | AFP

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa kaunti ya Kiambu ambayo ni ngome ya Rais Uhuru Kenyatta itashuhudia siasa za kukata na shoka.

Kwa sasa gavana Nyoro anaegemea upande wa Jubilee ambacho ni cha Rais Kenyatta.

Kwa hivyo inamaanisha atachukua mwelekeo wa chama cha Jubilee.

Kwa upande wake anajitetea akisema amefabikiwa kuleta maendeleo ya maji, afya, barabara, na kilimo. Haya yote  ametekeleza kwa miaka miwili aliyoshika usukani.

Naye Bw Wainaina pia kwa upande wake anadokeza kuwa amesaidia kuunda barabara mashinani.

Anajitetea pia kuhusu kuwahamasisha wakulima waanze kujishughulisha na kilimo bora cha macadamia, na kukarabati shule zaidi ya 25 za msingi, na kutoa fedha za maendeleo za basari kutoka ofisi za serikali.

  1. NG- CDF

Bw Waititu naye alijitetea kwa wananchi ya kwamba alibanduliwa ghafla kutoka kwa wadhfa wa ugavana na ana uhakika akipewa nafasi atakamilisha ajenda zake za maendeleo.

Bi Alice Ng’ang’a anayepania kugombea kiti cha ubunge cha Thika anasema hajasahau miradi aliyoendeleza, kwa hivyo anawarai wakazi wa Thika wamjaribu tena kwa mara ya pili ili akamilishe ahadi yake.

Hata hivyo wadadisi wa kisiasa wanadai kuwa ngoma ya kisiasa itashuhudiwa kamili wakati wa mchujo wa kutafuta tikiti kamili ya kuwania nacho uongozi.

Hapo ndipo tutashuhudia sokomoko ya wanasiasa kugura kutoka chama kimoja hadi lingine.

You can share this post!

Kheri ashauri vituo vya soka ya vijana vifufuliwe

Ni raha Jamal cup ikikamilika kwa mbwembwe nairobi

T L