Kimataifa

Vipimo vyabainisha viongozi kadhaa Afrika Kusini wanaugua Covid-19

July 18th, 2020 2 min read

PETER DUBE na CHARLES WASONGA

MAWAZIRI wawili zaidi nchini Afrika Kusini wamepatikana na virusi vya corona huku janga hilo likiendelea kushambulia watu kutoka tabaka la juu.

Waziri wa Madini na Kawi Gwede Mantashe na mkewe walithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo awali naye Waziri wa Uajiri na Leba akipatikana na virusi hivyo Ijumaa.

Kulingana na kitengo cha habari za serikali (GCIS) waziri Mantashe alipatikana na virusi vya corona baada ya kupimwa mara tatu tangu kuzuka kwa janga hilo mnamo Machi 2020.

“Waziri Mantashe na Bi Mantashe sasa ametengwa nyumbani na waziri ataendelea kufanya kazi kutokana huko,” taarifa hiyo ikaongeza.

Kuhusu Bw Nxesi, Msemaji wa Baraza la Mawaziri Phumla Williams alisema “ni mchangamfu na ana imani kwamba atapona.”

“Waziri Nxesi amejitenga na ataendelea kufanyakazi kutoka nyumbani. Wafanyakazi wote afisini mwake ambao walitangamana naye watapimwa kubaini ikiwa waliambukizwa au la,” akaongeza Bi Williams.

Maambukizi ya hivi punde yanajiri baada baada ya serikali kutangaza kuwa Waziri wa Ulinzi na Masuala ya Mashujaa wa Kivita Bi Nosiviwe Mapisa-Nqakula amepona Covid-19.

Mumewe Mpisa-Nqakula, Charles, ambaye ni mshauri wa masuala ya usalama katika Afisa ya Rais Cyril Ramaphosa, pia amepona baada ya kuugua homa hiyo.

Afrika Kusini inashuhudia idadi kubwa ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona ambavyo sasa vimetimu 337, 595 huku ikiwa imeandikisha vifo 4, 804.

Kwa wastani, jumla ya watu 12,000 wapya huambukizwa ugonjwa huo nchini Afrika Kusini, ambayo ilikuwa inashikilia nambari sita duniani kwa kiwango cha maambukizi kufikia Ijumaa.

Miongoni mwa wanaoambukizwa ni maafisa wa ngazi ya juu serikali.

Naibu Waziri wa Ustawi wa Kijamii Hendrietta Bogopane-Zulu anatibiwa nyumbani huku Nkosi Holomisa ambaye ni Naibu Waziri wa Haki na Huduma za Magereza amepona.

Maafisa wengine wa serikali ambao wamewahi kuambukizwa virusi vya corona ni Mkuu wa Mkoa wa Gauteng David Makhura na mwenzake kama vile Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi mwa Cape Job Mokgoro na Mkuu wa Mkoa wa Magharibi mwa Cape Alan Winde.

Watatu hao wametengwa nyumbani.