Habari

Viongozi Kwale wataka nafasi ya marehemu Tabwara irudi kaunti hiyo

December 30th, 2019 2 min read

Na MSHI GONGO na WACHIRA MWANGI

VIONGOZI katika Kaunti ya Kwale wamewaomba wakazi kudumisha umoja na kuepuka siasa zinazoweza kuwagawanya kwa misingi ya kikabila.

Viongozi hao wakiongozwa na Gavana wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya aidha wamemuomba Rais Uhuru Kenyatta kuchagua mkazi wa Pwani, kuchukua nafasi ya aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Mshikamano na Ushirikiano (NCIC) Bi Fatuma Tabwara aliyefariki Jumapili.

Akizungumza katika mazishi ya naibu huyo, gavana Mvurya amewahimiza wakazi kuchagua viongozi kuzingatia utaalamu walio nao na si kwa misingi ya kikabila au mirengo ya kisiasa.

“Watu wengi wameguswa na utaalamu aliokuwa nao Bi Tabwara. Kifo chake ni pigo kwa watu wa Kwale na Kenya kwa Jumla lakini tunaomba nafasi hii isalie katika kaunti ya Kwale,” akasema gavana Mvurya.

Marehemu Tabwara amezikwa Jumatatu eneo la Kombani Matuga, Kaunti ya Kwale.

Viongozi kutoka serikali kuu na zile za kaunti, pamoja na wakazi wamefurika nyumbani kwa marehemu kutoa heshima zao za mwisho.

Marehemu alizirai harusini alipokuwa amehudhuria, akawahiwa katika hospitali binafsi ya Diani Beach saa nne asubuhi lakini ikabainika kuwa alikuwa ameshafariki.

Mwenda zake ameacha mume Bw Fuad Said Gofwa, wasichana wawili na wavulana.

Miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni maafisa kutoka tume ya NCIC, katibu mkuu Prof Hamadi Boga, afisa wa tume ya ardhi Kazungu Kambi, wabunge Paul Kahindi Katana (Kaloleni), Kassim Tandaza (Matuga), Seneta wa Kaunti ya Kwale Issa Juma Boy, Kamishna wa Kaunti ya Kwale Karuku Ngumo.

Gavana Mvurya amemtaja marehemu kama kiongozi shupavu na mfano mwema katika jamii.

“Tuweke ndoto ya marehemu hai kwa kufuata aliyokuwa akitukumbusha kila siku. Tudumishe umoja na amani miongoni mwa jamii za Kwale,” amesema Mvurya.

Bi Wambui Nyutu akisoma salamu za pole kwa niaba ya tume ya NCIC ametaja kifo cha Bi Tabwara kuwa cha ghafla na cha kushtua.

“Marehemu ameacha pengo ambalo itakuwa vigumu kuliziba, itatuchukuwa muda mrefu sisi kama tume kukubali kifo chake,” amesema.

Bi Tabwara alihudumu katika tume hiyo kama naibu mwenyekiti kwa miezi miwili pekee lakini ametajwa kuwa alifanikiwa kuleta mabadiliko makubwa katika tume hiyo.

Bi Nyutu amemtaja marehemu Tabwara kama mzalendo aliyejitolea kuhudumia Wakenya mashinani na hata kitaifa bila kujali kabila wala dini.