Viongozi Mlima Kenya wampa Raila matakwa

Viongozi Mlima Kenya wampa Raila matakwa

Na JAMES MURIMI

VIONGOZI wa eneo la Mlima Kenya wamewasilisha kwa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, orodha ya mambo wanayotaka ili kuinua uchumi wa eneo lao kupitia biashara ndogo na za kati.

Magavana kutoka Muungano wa Kiuchumi wa Kaunti za Kati (CEREB) walimtaka Bw Odinga kuweka kipaumbele suala la ustawi wa biashara ndogondogo iwapo atashinda urais mwaka ujao.

Magavana hao Francis Kimemia (Nyandarua), Ndiritu Muriithi (Laikipia) na James Nyoro (Kiambu) walikutana na Bw Odinga katika hoteli ya Maiyan mjini Nanyuki, jana.

Bw Muriithi alisema kwamba walifanya mazungumzo ya kina na waziri mkuu huyo wa zamani jinsi ya kuimarisha uchumi wa kanda hiyo.

“Ukuaji wa uchumi ni lazima utegemee ustawi wa taasisi zetu za kiuchumi wala sio kuhonga watu,” alieleza Bw Muriithi.

Gavana huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza la Magavana (CoG), alisema kuna haja ya kupigajeki biashara ndogo na pia kuwapa vijana uwezo wa kujikimu kimapato kupitia ugavi sawa wa fedha.

Vilevile, viongozi hao walijadili jinsi ya kumaliza mavamizi ya kila mara ya majangili katika Kaunti ya Laikipia na kaunti zingine jirani.

“Usalama ni muhimu kwa maendeleo katika jamii. Ni jukumu la serikali kulinda maisha na mali ya Wakenya wote,” alihoji Bw Odinga.Magavana hao walisema kuwa wataendelea kukutana na Bw Odinga kujadili maslahi ya eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

“Tutapanga na kushiriki mazungumzo ya eneo hili tukilenga viongozi waliochaguliwa, viongozi wa kijamii, viongozi wa kidini, viongozi wa kibiashara, mashirika ya wakulima na wadau wengine mbalimbali kuhusu maslahi ya eneo letu. Mwindaji aliye makini hafanyi majadiliano kando ya barabara,” akasema Bw Muriithi.

Aliongeza: “Huu ni mkutano wa kwanza katika msururu wa vikao kadha ambavyo tumepanga eneo hili. Vitaishia kwa kutangaza azimio la ukanda.”

Bw Odinga alisisitiza kuwa chama chake cha ODM kitashirikiana na vyama vya kisiasa kutoka Mlima Kenya kupiga jeki azma yake ya kugombea urais. Kwenye ziara yake ya siku tatu, waziri huyo mkuu wa zamani alikutana na viongozi wa vyama vya PNU na KANU kutoka eneo hilo na kuahidi kushirikiana.

Aidha, alisema ataendelea na mikutano kote nchini akijiandaa kwa uchaguzi mkuu 2022. Juzi, kaunti wanachama wa CEREB ziliafikiana kuwa wafanyabiashara, watengenezaji bidhaa na watoaji huduma katika maeneo yao watahitajika kuwa na leseni moja tu ya kaunti mwanachama, ili kuondoa vikwazo vya ushuru vinavyozuia ustawi wa biashara.

You can share this post!

Joho atiwa presha atangaze mrithi wake

EPRA yashikilia kuwa ushuru na bei ya mafuta ng’ambo...