Viongozi Mlima Kenya watazuru Nyanza kuthibitisha wanaunga mkono Raila – Orengo

Viongozi Mlima Kenya watazuru Nyanza kuthibitisha wanaunga mkono Raila – Orengo

Na MWANDISHI WETU

UJUMBE wa viongozi waliochaguliwa eneo la Mlima Kenya utazuru Nyanza kuthibitishia wenyeji kwamba ngome ya Rais Uhuru Kenyatta itamuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, seneta wa Siaya, James Orengo amefichua.

Bw Orengo alisema ana uhakika eneo la Mlima Kenya litamuunga Bw Odinga katika azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka ujao.

“Ili kuthibitisha kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Bw Odinga, tutawaleta wabunge na maseneta kutoka eneo la Kati hapa Nyanza kuwadhihirishia watu kwamba kwa hakika wako nyuma yake,” alisema akiwa eneo la Usigu, Bondo Kaunti ya Siaya.

Mwaka jana, kundi la wazee kutoka eneo la Mlima Kenya na baadhi ya wanasiasa walimtembelea Bw Odinga nyumbani kwake Siaya ambako walikutana na wazee wa jamii ya Waluo.

Seneta Orengo ambaye ni mmoja wa washirika wa karibu wa Bw Odinga alisema kwamba makaribisho ambayo waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa akipokea eneo la Kati hivi majuzi ni dhihirisho kwamba limeamua kumkumbatia.

Bw Odinga amezuru eneo la Kati mara kadhaa mwaka huu katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono.Wiki jana, Bw Odinga alihutubia mikutano kadhaa ya kisiasa eneo la Kati akitoka Laikipia alipokutana na baadhi ya magavana na wabunge walioahidi kumuunga mkono.

Wiki hii, alikutana na mabwanyewe wa eneo hilo walioashiria kwamba wataunga mkono azma yake ya kumrithi Rais Kenyatta.

Bw Orengo alipuuza madai kwamba Rais Kenyatta atamsaliti Bw Odinga akifafanua kuwa uhusiano wao wa karibu unaonyesha kwamba kiongozi wa nchi anaunga azma ya Odinga.

Viongozi hao wawili wamekuwa na uhusiano wa kirafiki tangu handisheki yao mnamo Machi 9, 2018 iliyotuliza joto la kisiasa nchini baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Akizungumza alipoongoza kampeni ya vijana kuchukua vitambulisho katika kituo cha afya cha Usigu Ijumaa, Bw Orengo alihakikishia wakazi kwamba kura za Bw Odinga hazitaibwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Chama cha ODM kimekuwa kikishikilia kwamba Bw Odinga amekuwa akipokonywa ushindi katika chaguzi tatu alizowahi kugombea urais.

Bw Orengo alisema kwamba viongozi wa Nyanza wanazingatia sana siasa za kitaifa ili kuhakikisha Bw Odinga ataingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na Bw Orengo, hakutakuwa na kitu cha maana kufaidi wakazi wa Nyanza iwapo Bw Odinga hatashinda urais.

Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda ambaye aliandamana na Bw Orengo aliwahimiza wakazi kujisajilisha kwa wingi kama wapigakura kwa kuwa hiyo ndio njia ya pekee ya kuhakikisha wanachagua viongozi wanaowapenda.

Alikubaliana na Bw Orengo kwamba nyadhifa za uongozi eneo la Nyanza hazitakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi iwapo Bw Odinga hatakuwa rais.

You can share this post!

Mshirika wa karibu wa Shahbal ahamia UDA

Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka