Makala

Viongozi Murang’a wasema Waziri Linturi ‘amechoma’ vya kutosha

April 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi katika Kaunti ya Murang’a wamemuonya Rais William Ruto kwamba Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi anapotezea serikali umaarufu katika eneo la Mlima Kenya.

Viongozi hao wakiongea Aprili 12, 2024 mjini Maragua wakati wa kutuza walemavu na magari spesheli ya kuwawezesha kusafiri, walimtaka Rais Ruto afanye hima kumchunguza waziri huyo kufuatia suala tata la mbolea feki.

Aidha, viongozi hao wa kisiasa wanapendekeza atimuliwe kazini endapo atapatikana na hatia.

“Hatufai tena kuogopa kusema wazi kwamba waziri huyu amelemewa na kazi kwa kuwa fatalaiza feki imeletwa mashinani chini ya uratibu wa mwongozo wake. Uwajibikaji ni wake. Fatalaiza hiyo imetupiga vita sana mashinani na Rais Ruto hafai kuchukulia suala hilo kama la mzaha,” akasema mbunge mwakilishi wa Murang’a, Betty Maina.

Bi Maina alisema kwamba “eneo la Meru lina watu wengi ambao wanaweza kufanya kazi bora kwa wakulima kuliko Bw Linturi na wakati wa mabadiliko katika wizara hiyo umewadia”.

Bi Maina alisema kwamba “kufikia sasa Waziri Linturi hajakuwa na mwito wa kufika mashinani Mlima Kenya kuhamasisha wakulima kukumbatia mbinu faafu kuwaongezea mapato”.

Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua alisema kwamba kazi ya kutetea Rais na serikali mashinani imegeuka kuwa ngumu kutokana na utepetevu wa Wizara ya Kilimo.

“Mimi nimetembelea mabohari ya nafaka yaliyo mji wa Maragua na nimekumbana na mahangaiko tele ya wakulima wakitafuta mbolea hiyo ya ruzuku. Kazi ya Bw Linturi ina dosari,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba Bw Linturi anafaa achunguzwe na akipatikana na hatia, apigwe kalamu.

“Hatuwezi tukakaa hapa mashinani tukijaribu kuwapa wakulima motisha na imani huku nayo wizara ya Linturi ikituangusha kwa kuwaletea mbolea iliyojaa kinyesi cha punda na mbuzi. Hujuma ya aina hiyo inafaa itekelezewe uchunguzi wa kina na aliye kwa lawama abebeshwe mzigo wa adhabu,” akasema.

Hata hivyo, Bw Linturi ambaye bunge la kitaifa pia limetishia kumng’oa mamlakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye amesema kwamba hakuna kashfa kubwa katika suala hilo.

Amejitetea kwamba ni magunia 3, 000 tu ambayo yalikuwa ya ubora duni wala sio kwa kiwango kinachosemwa na wengi nchini.

Huku akisema kwamba tayari kampuni iliyohusishwa na kashfa hiyo imepokonywa leseni na kandarasi yake kufutiliwa mbali, Linturi aidha alisema uchunguzi zaidi utaishia baadhi ya washukiwa kushtakiwa.