Michezo

Viongozi na wakazi wa Ruiru walalamika kuhusu ubovu wa barabara

December 10th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa mtaa wa Membley na viongozi wa eneo hilo wamelalamika jinsi barabara ya kilomita sita imejengwa kwa mwendo wa kobe.

Viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara walisema ya kwamba mwaka uliopita mwezi Julai, 2019, rais Uhuru Kenyatta alipozuru Ruiru alitoa amri barabara hiyo iliyogharimu Sh235 milioni ijengwe mara moja.

Barabara hiyo ilikuwa inaunganishwa na Thika Superhighway- Membley Mashariki ikipitia kahawa Magharibi na kufika chuo cha mafunzo cha Bible Literacy College mjini Ruiru.

Ilidaiwa kuwa mhandisi anayekarabati barabara hiyo amefanya asilimia mbili pekee ya kazi hiyo jambo ambalo viongozi hao walitaja kama kutotimiza ahadi ya kazi hiyo.

Baadhi ya viongozi ambao wametoa malalamishi yao ni Bw Simon King’ara (Ruiru), Gathoni Wa Muchomba (Kiambu), na Isaac Mwaura (seneta maalum wa Jubilee).

Bw King’ara aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kushirikiana na wahandisi hao ili kufanikisha kukamilika kwa kazi hiyo.

Alimshauri mhandisi mkuu wa mradi huo kufanya juhudi kuona ya kwamba kazi zote zinapewa wakazi wa Ruiru badala ya watu kutoka mbali kupewa kazi.

” Sisi hatuko tayari kwa mivutano na mhandisi bali tunataka kufanya kazi kwa njia ya uelewano,” alisema Bw King’ara.

Bi Wamuchomba ( mbunge wa Kiambu,) ambaye ni naibu wenyekiti wa uchunguzi katika kamati ya bunge aliwataka wahandisi hao watimize ahadi yao ya kukamilisha kazi hiyo haraka iwezekanavyo.

” Kuna baadhi ya viongozi wanaoishi katika eneo ambalo barabara hiyo inajengwa na kwa hivyo tunapitia masaibu mengi,” alisema Bi Wa Muchomba.

” Mara nyingi huwa sifungui madirisha katika jumba langu kwa sababu ya vumbi tele,” alifafanua.

Alitoa mwito kwa wahandisi kufanya kazi hiyo haraka ili magari yaweze kupata nafasi ya wazi kupitia eneo hilo.

Bw Mwaura naye alitaka pia mradi huo uharakishwe ili magari yapate njia bora ya kupitia.

Alisema mradi huo ukikamilika usafiri wa mabasi utaimarika pakubwa pamoja na magari madogo.

Viongozi hao walizuru eneo hilo mnamo Jumatano walipotaka kujionea jinsi mradi huo umeendeshwa kwa mwendo wa Kobe.

Hata hivyo alisema majira ya mvua kama wakati huu wakazi wa eneo hilo hukosa amani kwa sababu maji mengi hufurika hadi kwenye manyumba kadha.