Viongozi Pwani watafutia Ruto mgombea mwenza

Viongozi Pwani watafutia Ruto mgombea mwenza

Na ANTHONY KITIMO

WAFUASI wa Naibu Rais William Ruto katika ukanda wa Pwani, wameanzisha mipango ya kumtafuta kiongozi wa eneo hilo atakayeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wanasiasa hao wa mrengo wa Tangatanga eneo la Pwani walikutana siku nzima Jumapili, wakaamua kuunda jopo la wataalamu wa kisiasa na kiuchumi ambalo limetwikwa jukumu la kutoa mwongozo utakaowasilishwa kwa Naibu Rais hivi karibuni.

Mkutano huo ulionekana kuchochewa na jinsi Dkt Ruto alivyokutana majuzi na wanasiasa wa eneo la kati ambao pia wana matakwa yao, ikiwemo kumtaka ateue mmoja wao kuwa mgombea mwenza na vile vile aahidi kuinua uchumi wa eneo lao.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari, wanasiasa hao wa Pwani walisema wanatarajia kukutana na Dkt Ruto hivi karibuni kuwasilisha matakwa yao.Mkutano wao wa kisiri ulikuwa umeitishwa na Wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Khatib Mwashetani (Lungalunga) na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Wabunge Mohamed Ali (Nyali), Benjamin Tayari (Kinango), Sharrif Athman (Lamu Mashariki), Feisal Bader (Msambweni), Rehema Hassan (Tana River), Maseneta Anwar Loitiptip (Lamu) na Juma Wario (Tana River), aliyekuwa gavana wa Taita Taveta John Mruttu, na wataalamu mbalimbali ni miongoni mwa walioalikwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, Prof Hassan Mwakimako na mtaalamu wa masuala ya kijamii, Bi Umra Omar ndio watakaosimamia kamati maalumu.

Kamati hiyo itabuni mwongozo wa kustawisha uchumi wa Pwani na kupendekeza jinsi mwongozo huo utakavyotekelezwa endapo Dkt Ruto atashinda urais 2022 kupitia kwa vuguvugu lake la ‘Hustler’.

“Kamati itapendekeza mbinu za kujadiliana na kikundi cha Hustler kwa lengo la kujenga vuguvugu imara, lililo na mshikamano na uwezo wa kuleta mabadiliko ambalo litabadili mfumo wa kiuchumi Kenya,” ikasema taarifa hiyo.

Mapema mwaka huu, baadhi ya wanasiasa wa Tangatanga eneo hilo walidokeza kumpendekeza Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya awe mgombea mwenza wa Dkt Ruto.

Juhudi za Pwani kuunda muungano mmoja wa kisiasa zimeendelea kugonga mwamba kwani Gavana wa Mombasa Hassan Joho naye anapanga kushindania tikiti ya ODM ili kuwania urais.

Viongozi hao wa Pwani wananuia kushinikiza mwongozo wao uwe sehemu ya manifesto ya Dkt Ruto atakapowania urais.Kuhusu uteuzi wa mgombea mwenza, walikubaliana kuwa mmoja kati yao ndiye atateuliwa kwa kuzingatia uwezo wake kisiasa na kimaendeleo, na maadili yake pamoja na mahitaji mengine hasa yatakayomwezesha kutetea siasa zisizo za ukabila ili kuwezesha utendaji wa haki kitaifa.

“Uteuzi hautanuia kutenga kikundi chochote kile kingine, bali kumpa Naibu Rais Ruto nafasi ya kuchagua aliye bora zaidi kuwa mgombea mwenzake kutoka kwa orodha ya watu wenye uwezo,” ikaeleza taarifa yao.

Hivi majuzi, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa Mlima Kenya kujadiliana kuhusu mbinu bora ya kutatua changamoto za wakazi wa Mlima Kenya.

Katika mkutano huo, ilibainika kuwa mojawapo ya mbinu zilizopendekezwa ni kwamba, endapo Dkt Ruto atafaulu kuunda serikali ijayo, afuate nyayo za Rais Mstaafu Mwai Kibaki kufufua uchumi uliozorota wakati wa utawala wake na Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Walioteleza KCPE wawika katika KCSE

Watahiniwa watumia mbinu mpya za wizi KCSE