Habari Mseto

Viongozi sasa walia Rais amewatenga Wapwani

January 18th, 2020 2 min read

SIAGO CECE na CHARLES LWANGA

WANASIASA wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wachanganuzi wa siasa na viongozi wa kidini katika eneo la Pwani, wamemlaumu Rais Uhuru Kenyatta, wakidai alitenga eneo hilo kwenye hotuba aliyotoa majuzi kuhusu mwelekeo wa nchi.

Viongozi hao walisema kuwa Rais Kenyatta amelitenga eneo hilo, hasa kwenye juhudi zake katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Viongozi wa kidini pia walisema kuwa eneo hilo halikuwakilishwa ifaavyo kwenye mageuzi aliyofanya majuzi kwenye baraza la mawaziri.

Kwenye hotuba aliyotoa mnamo Jumanne katika Ikulu ya Mombasa, Rais alieleza lengo lake katika kuimarisha sekta za majanichai, kahawa, ndizi na kilimo cha mpunga.

Rais pia alitoa agizo kwa Hazina ya Kitaifa kutoa Sh300 milioni kwa Mamlaka ya Kusimamia Biashara Ndogo Ndogo (MSEA) kufadhili ujenzi wa mitambo ya kuhifadhi mazao katika kaunti za Nyandarua, Meru na Kisii. Walisema eneo hilo halikujumuishwa kwenye mikakati hiyo.

Wabunge Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na Aisha Jumwa (Malindi), walisema kuwa jamii ya Wamijikenda haikujumuishwa kwenye mageuzi hayo. Wawili hao walitoa jumbe kali za kumkosoa Rais Kenyatta, ambazo baadaye waliziweka katika mitandao ya kijamii.

Wawili hao walimwambia Rais akumbuke kwamba anawaongoza Wakenya milioni 47 na si jamii kadhaa.

Kupitia kanda ya video, Bi Jumwa alisema kuwa alishangazwa na jamii ya Wamijikenda kutojumuishwa katika mageuzi hayo, licha ya handisheki na ripoti ya Jopo la BBI kushinikiza umoja miongoni mwa Wakenya.

Bi Jumwa ni miongoni mwa viongozi ambao wamejitokeza wazi kuunga mkono nia ya Dkt Ruto kuwania urais mnamo 2022.

“Nimeshangaa kwamba umoja huu ambao wamekuwa wakiuzungumzia umewaacha Wamijikenda. Je, wao si Wakenya?” akasema, akiongeza kuwa yeye si mkabila.

Athari za SGR

Kwa upande wake, Bw Baya alisema kuwa licha ya Rais kutangaza mikakati hiyo jijini Mombasa, ni kinaya kwani hakugusia changamoto za kiuchumi zinazolikabili eneo hilo kama athari za Reli ya Kisasa (SGR) kwa kampuni za usafirishaji mizigo.

“Rais alionyesha kuwa pengine hana mpango wowote kuhusu kulistawisha eneo hili kiuchumi wala kujumuisha viongozi wake kwenye baraza la mawaziri. Jamii ya Wamijikenda haikupata uteuzi wa hata wadhfa mmoja. Tunahisi kutokuwa sehemu ya Kenya,” akasema.

Msimamo huo wa wafuasi wa Dkt Ruto unaonekana kushika kasi wakati ambapo Naibu Rais ameonekana kuongeza ziara zake katika eneo la Pwani.

Wiki jana, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa kaunti ya Taita-Taveta na kujadiliana masuala mbalimbali.

Haijajulikana moja kwa moja kama juhudi hizo zina athari yoyote itakayofanikiwa kutingisha ngome ya chama cha ODM ukanda wa Pwani.

Bi Jumwa na Bw Baya wanatoka kaunt i ambayo wabunge wote saba ni wa chama cha ODM.

Hata hivyo, baadhi ya wenyeji waliwakosoa vikali, wakisema kuwa Rais Kenyatta amewateua viongozi wawili kutoka jamii hiyo serikalini, wakiwemo Naibu Waziri katika Wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu.