Habari za Kaunti

Viongozi Taita Taveta wataka kaunti idhibiti mapato kutoka mbuga ya Tsavo

May 15th, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

BAADHI ya viongozi wa Kaunti ya Taita Taveta wameanzisha mjadala mpya kuhusu usimamizi wa Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo, wakidai mabadiliko katika mfumo wa ugavi wa mapato.

Wakiongea mjini Mwatate, wawakilishi wa bunge la kaunti hiyo wamejitenga na mfumo wa sasa wa ugavi wa nusu ya mapato ya hifadhi hiyo, wakipendekeza badala yake mbuga hiyo igatuliwe ili kudhibitiwa moja kwa moja na kaunti hiyo.

Mjadala huu unajiri kufuatia mvutano unaoendelea kuhusu kanuni ya ugavi wa mapato ya kitaifa, ambapo Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa akishinikiza mfumo wa ‘mtu mmoja, kura moja, shilingi moja’.

Mfumo huo, unaopendelea idadi ya watu badala ya ukubwa wa eneo, umekumbana na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa Taita Taveta, ambao wanahisi kwamba unapendelea kaunti zilizo na idadi kubwa ya watu.

Wawakilishi hao walielezea kutoridhishwa kwao na mfumo uliopendekezwa, wakisisitiza kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya kaunti inamilikiwa na hifadhi ya wanyamapori ya Tsavo.

Mbuga ya Tsavo inamiliki zaidi ya asilimia 62 ya ardhi ya Taita Taveta.

Mwakilishi maalum Bw Peter Shambi alisema, kuwa serikali kuu itafinyilia Taita Taveta yenye uchache wa watu wa idadi 350,000.

“Serikali inataka kutubagua. Naibu Rais ameahidi eneo la Mlima Kenya kuwa atahakikisha mfumo wa mtu mmoja, kura moja, shilingi moja’ unapita, lakini njia hiyo haitutendei haki,” akasema.

Bw Shambi alisema kuwa kaunti hiyo haitaunga mkono mfumo huo na hivyo kukaza kamba ili kuhakikisha kuwa harakati zao za kudhibiti mbuga ya Tsavo inatimia.

“Hatua hii itasaidia kaunti yetu kupata mapato zaidi na kujikwamua kutokana na ufadhili duni wa serikali ya kitaifa. Tutaweza kukuza mapato yetu kwa kuwa tutasimamia rasilimali zote zilizomo humo,” alisema.

Mwezi Aprili, Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ilianza kushirikisha umma katika kutafuta mfumo wa nne wa ugavi mapato ya nchi.

Bw Shambi pia alielezea masikitiko yake kuhusu ahadi za viongozi wa serikali ya kitaifa kuhusu mapato ya Tsavo, ikiwemo ahadi ya Rais William Ruto ya kugawana mapato hayo 50-50, ambayo bado haijatekelezwa.

“Rais aliahidi, lakini Waziri wa Utalii alisema haiwezekani. Hatutachoka hadi tuone kuwa mbuga hii inagatuliwa,” alisema.

Bunge la kaunti hiyo lilipitisha hoja ya kutuma ombi kwa bunge la kitaifa kufanyia marekebisho Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori, likilenga kubadilisha mbuga hiyo kuwa hifadhi ili kusimamiwa na serikali ya kaunti.

Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti katika bunge la kaunti Bw Jimmy Mwamidi, ambaye alifadhili hoja hiyo, alisema marekebisho hayo yataleta usawa wa kiuchumi kwa kaunti hiyo, ambayo imenyanyaswa kifedha licha ya mbuga hiyo kuchukua sehemu kubwa ya ardhi yao.

Uamuzi huo ulijiri baada ya Waziri wa Utalii na Wanyamapori Alfred Mutua kudokeza uwezekano wa kuangaliwa upya kwa ahadi ya mgao wa mapato ya 50-50 kutoka Tsavo iliyotolewa na Rais Ruto Julai mwaka jana.

Aidha, Gavana Andrew Mwadime pia amekuwa akipinga mfumo wa ugavi unaopendekezwa na baadhi ya kaunti za idadi kubwa ya watu, akisema unanyima kaunti kama Taita Taveta rasilimali zinazostahili.

Alitoa wito wa kuongezwa kwa mgao kutoka kwa serikali ya kitaifa akisema itawezesha kaunti hiyo kutimiza malengo yake ya kimaendeleo.

“Ikiwa mfumo huo utatekelezwa, hakutakuwa na usawa katika ugavi wa rasilimali za kitaifa. Mfumo huo umekandamiza kaunti zilizotengwa tangu jadi,” alisema.