Habari Mseto

Viongozi wa dini ya Kiislamu waendeleza kampeni kupigana na ugaidi Pwani

January 31st, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MUUNGANO wa Usimamizi wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu (AMP) eneo la Pwani umejitolea kuendeleza kampeni kabambe ya kupiga vita mafundisho ya itikadi kali na ugaidi miongoni mwa waumini, vijana na wananchi kwa jumla.

Kampeni hiyo ambayo ilianza tangu 2014 baada ya mashambulio ya wapiganaji wa al-Shabaab kushuhudiwa kwenye miji ya Mpeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi, ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa na mali ya mamilioni ya fedha kuharibiwa, pia inalenga kuleta uwiano, utangamano na kujenga imani zaidi miongoni mwa wakazi wa makabila mbalimbali yanayoishi kwenye kaunti zote sita za Pwani.

Wakati wa kikao maalum kilichoandaliwa kwenye ukumbi wa jumba la Huduma Centre mjini Lamu na kuleta viongozi mbalimbali wa kidini, kijamii, wakuu wa usalama na wanaharakati, mkurugenzi wa muungano huo wa AMP, Sheikh Khamisi Libondoh, alikosoa baadhi ya viongozi wa kidini na vijana ambao wamekuwa wakitafsiri neno ‘Jihadi’ kwa njia isiyostahili.

Kulingana na Sheikh Libondoh, Jihadi ni wajibu tu wa kidini katika Uislamu, ambapo waumini wanatarajiwa kujitahidi kutenda yanayostahili, hasa yale yaliyo mema kwa ajili ya Allah.

Sheikh Libondoh alisema ni jambo la kusikitisha na kinyume cha dini yoyote kuona kwamba vijana, hasa wale waliopokea mafundisho ya itikadi kali na hata kujiunga na makundi ya kigaidi kuendeleza harakati mbovu za kuua wananchi wasiyo na hatia kwa kusingizia Jihadi.

Aliwataka vijana na hata viongozi wa kidini misikitini kujiepusha na mafundisho ambayo yanakinzana na mambo halisi yaliyoko ndani ya Quran na Uislamu kwa jumla.

“Furaha yetu ni kuona wananchi, ikiwemo wasilamu na wale wasio waislamu wanaishi vyema, wakishirikiana na kupendana. Wale wanaofuata mafundisho yasiyostahili na ambayo ni kinyume ya Uislamu ni wahalifu. Kuna wanaojiunga na makundi ya kigaidi eti kwa kisingizio kwamba wanamtetea Allah. Wanaendeleza mauaji ya watu wasio na hatia. Hicho ni kinyume cha dini yoyote na lazima tusimame wima kupinga jambo hilo,” akasema Sheikh Libondoh.

Aliyekuwa mgeni rasmi na msemaji mkuu wakati wa kongamano hilo, Sheikh Mohamud Mau,alisema ipo haja ya wakazi kuishi kwa upendo na kupiga vita yeyote anayewajia akitaka kuwagawanya, iwe ni kwa misingi ya kidini au hata kikabila.

Dini ya amani

Alishikilia kuwa dini ya Kiislamu ni ya amani na pia imekuwa mstari wa mbele kueneza amani hiyo kote nchini.

“Hata maamkuzi yenyewe ya kiislamu yanaashiria amani. Anayejidai kuwa Mwislamu lakini vitendo vyake vinakinzana na yanayopaswa kufanywa katika Uislamu huyo si wa dini hiyo. Tuwe imara kumpinga yeyote anayevuruga amani yetu na kutugawanya kwa misingi yoyote ile,” akasema Sheikh Mau.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa divisheni ya Amu, Bw Philip Oloo alitaja ugaidi kuwa tatizo la ulimwengu mzima linalohitaji juhudi za kila mmoja ili kulishinda tatizo hilo.

Aliwataka vijana kujiepusha na makundi yoyote ya uhalifu na badala yake kujitahidi kuwa raia wema kwa maendeleo ya nchi hii.