Viongozi wa Gusii mbioni kuunda chama chao cha siasa

Viongozi wa Gusii mbioni kuunda chama chao cha siasa

Na WYCLIFFE NYABERI

KINARA wa ODM, Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto, wanakabiliwa na kibarua kipya cha kuishawishi jamii ya Abagusii iwaunge mkono uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii inafuatia hatua ya wabunge wa eneo hilo kudokeza kwamba kuna uwezekano wakaunda chama chao kimoja.

Katika mkutano wa Alhamisi jijini Nairobi, wabunge wapatao 15 kutoka eneo hilo waliafikiana kuweka tofauti zao kando ili kushawishi jamii hiyo kuzungumza kwa sauti moja kisiasa.

Japo wabunge hao wanatoka vyama tofauti, wamekuwa wakionyesha hadharani kuwa kuna wale wanaoumuunga mkono Dkt Ruto na wengine wakimshabikia Bw Odinga.

Katika taarifa ya pamoja, wabunge hao walidokeza kuwa watachambua wawaniaji wote wa urais ili kutathmini atakayeifaa jamii hiyo zaidi.

“Ikiwa vyama vilivyopo na wawaniaji hawatatimiza matakwa yetu kama Wakisii, basi tutakuwa radhi kuunda chama tutakachokikuza,” akasema mbunge wa Borabu, Bw Ben Momanyi.

Mbunge wa Mugirango Kusini, Bw Silvanus Osoro, alidokeza kwamba kwa miaka mingi jamii hiyo imekuwa ikialikwa kwenye “majumba ya kupanga kisiasa” ila wakati huu ni lazima wahusishwe kikamilifu.

“Ni vyema ijulikane kwamba raundi hii hatutakuwa watazamaji bali washirika. Hatutakuwa wachezaji wa akiba wanaokaa kwenye benchi; lazima tuhusishwe kwenye mchezo,” Bw Osoro akasema.

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw Simba Arati, naye alisema wana imani kuwa juhudi zao zitazaa matunda.

“Kwa hakika msimu huu ni lazima tutembee katika gari moja. Mkate utakapokuwa ukigawanywa, nasi pia tungependa kupata sehemu yake. Kwa kuja pamoja tutasaidia kuleta maendeleo mengi Gusii,” Bw Arati alieleza.

Mbunge wa Mugirango Kaskazini, Bw Joash Nyamoko, alidokeza kwamba kuja kwao pamoja kumekumbatia maoni tofauti ya washikadau wote.

Wabunge wengine waliokuwepo katika mkutano wa Nairobi ni Naibu Kiongozi wa Wengi Bunge la Kitaifa Bw Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kaskazini), Bw Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini), Bw Zadoc Ogutu (Bomachoge Borabu), Bw Jerusha Momanyi (Mwakilishi wa Kike Nyamira), Bw Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi), Bw Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba), Bw Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi), Bw Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Bw Richard Tong’i (Nyaribari Chache), Bw Alfa Miruka (Bomachoge Chache), Bi Millicent Omanga (Seneta Mteule) na Bw Innocent Obiri (Bobasi).Maseneta Sam Ongeri (Kisii), Okong’o Omogeni (Nyamira ) na Mwakilishi wa Kike Kisii Janet Ong’era hawakuhudhuria.

You can share this post!

Wazee wa Nyumba 10 wadai mshahara

NHIF yapunguza pesa za dialisisi, CT-Scan