Viongozi wa Homa Bay wataka Raila awapelekee minofu katika ziara yake eneo hilo

Viongozi wa Homa Bay wataka Raila awapelekee minofu katika ziara yake eneo hilo

NA GEORGE ODIWUOR

VIONGOZI wa Homa Bay wamemtaka mgombea urais wa Azimio Raila Odinga awasaidie kufanikisha miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.

Leo Jumamosi Bw Odinga anatarajiwa kuzuru kaunti hiyo kupigia debe azma yake ya urais.

Hii ni baada ya mgombea mwenza wake, Martha Karua, kuzuru Homa Bay Jumatano ambapo alitoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Bw Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9.

Lakini tofauti na ziara ya Bi Karua iliyotawaliwa na siasa, viongozi wa eneo hilo sasa wanataraji kuwa Bw Odinga atawapelekea mazuri kimaendeleo.Viongozi wa kaunti hiyo wameorodhesha mambo ambayo wangemtaka Bw Odinga aangazie anapozuru eneo hilo.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero, ambaye anawania kiti cha ugavana wa Homa Bay alisema Bw Odinga anafaa kutumia ushawishi wake katika serikali ya Jubilee kuwafaidi wakazi wa Homa Bay.

Tangu Machi 9, 2018 Bw Odinga aliporidhiana kisiasa na Rais Kenyatta, eneo la Nyanza limefaidi kwa miradi kadha ya maendeleo kama vile kufufuliwa kwa uchukuzi wa ziwani Victoria na uchukuzi wa reli.

Aidha, viwanda kadha vimeanzishwa kama vile cha kutengeneza meli, ukarabati wa fuo katika Ziwa Victoria miongoni mwa miradi mingine.

Dkt Kidero alisema miradi mingine ya maendeleo inaweza kuanzishwa katika eneo hilo ikiwa viongozi watawasilisha matakwa yao kwa serikali.

“Kupitia kwa Bw Odinga, matakwa ya maendeleo ya Homa Bay yanaweza kupitishwa kwa Rais Kenyatta,” akasema Dkt Kidero.

Alisema Bw Odinga anaweza kushinikiza kupandishwa hadhi kwa Chuo Kikuu Kishirikishi cha Tom Mboya kuwa chuo kikuu kamili.

Mpango ya kupandishwa hadhi kwa chuo hicho chenye wanafunzi 3500 umekuwepo lakini haujatekelezwa.

“Tungetaka Waziri Mkuu kumwomba rais aipe chuo hiki cheti cha utambulisho ili kikome kuwa chuo bewa ya Chuo Kikuu cha Maseno bali Chuo Kikuu kinachojisimamia,” Dkt Kidero akaongeza.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo Nyandiko Ongadi aliwataka wanasiasa wa kaunti hiyo kutumia ziara ya Bw Odinga kama nafasi ya kuitisha miradi ya maendeleo wala sio kuendeleza ajenda za kuwanufaisha pekee.

  • Tags

You can share this post!

Wasanii wa Kayole kuzindua filamu mpya mwezi huu wa Julai

Mikakati ya Nassir kufufua uchumi Mombasa

T L