Habari MsetoSiasa

Viongozi wa Jubilee wakashifu Murathe na Tuju

April 24th, 2020 2 min read

Na GITONGA MARETE

VIONGOZI wa Chama cha Jubilee kutoka Kaunti ya Meru ambao ni wandani wa Naibu Rais, Dkt William Ruto wameapa kwamba watapigana vikali kudhibiti chama hicho ambacho kwa sasa kinakumbwa na mzozo wa uongozi kati ya mirengo miwili pinzani.

Wanasiasa hao pia walimshutumu Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti David Murathe kwa kuendesha chama hicho kama mali yao ya kibinafsi.

Kiini cha mzozo wa Jubilee ni uhasama kati ya mrengo wa Dkt Ruto na Mabw Tuju na Murathe ambao wanaaminika kuwa na ‘baraka’ za Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Tuju hivi majuzi alimwandikia msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu akipendekeza maafisa wa chama wabadilishwe na hata kutoa orodha ya washikilizi wapya wa nyadhifa chamani lakini suala hilo likapingwa na wafuasi wa Dkt Ruto.

Upande wa Naibu Rais ulisisitiza kuwa hakuna mkutano wa Baraza Kuu la Chama ulioidhinisha mabadiliko aliyoyapendekeza Bw Tuju.

Seneta wa Meru Mithika Linturi ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa kundi la wabunge wa Kaunti ya Meru, jana alisema wamewekeza sana na kuunga chama hicho tangu kiundwe ndiyo maana hawatakubali kinyakuliwe na mrengo unaopinga Dkt Ruto.

Bw Linturi aliahidi kwamba watatumia njia zote kusalia na chama hicho ikiwemo kuelekea mahakamani kupinga juhudi zozote za kukibinafsisha kwa wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta pekee.

“Tunaendelea kushauriana kuhusu hatua tunayopaswa kuchukua. Binafsi mimi huchanga Sh10,000 kila mwezi kama mwanachama wa Jubilee na hatutawaruhusu Bw Tuju na Bw Murathe kudhibiti chama hiki. Tutapigana vita hivi kwa njia zote hadi tushinde,” akasema Bw Linturi.

“Chama cha Jubilee kina wanachama na hakifai kuendeshwa kama kioski. Ni kama kampuni ambayo wanachama wana hisa isiyofaa kumilikiwi na watu binafsi. Mtu yeyote anayefikiri kwamba atadhibiti chama, anajidanganya bure. Hawana mamlaka ya kufanikisha mabadiliko yoyote na tutasitisha mipango yao liwalo na liwe,” akaongeza.

Wabunge Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini) nao waliwashutumu wawili hao kwa kujihusisha na siasa wakati ambapo taifa linapigana na janga la virusi vya corona.

Wabunge hao waliwataka wawili hao wakomeshe chuki na uhasama dhidi ya viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto.

Waliwashutumu Bw Tuju na Bw Murathe kwa kumpotosha Rais na kumfanya asimakinikie vita dhidi ya corona ambayo sasa inatishia kuharibu uchumi wa nchi.

Bw Dawood naye alishikilia kwamba kimya cha Rais Kenyatta kuhusu utata unaozingira kubadilishwa kwa maafisa wa chama kinafaa kufasiriwa kwamba upande wa Naibu Rais ndio msema-kweli.

“Naibu kiongozi wa chama chetu ni Dkt Ruto na tunatii kile anachosema. Rais Kenyatta hataki kuhusishwa na siasa za chama kwa sababu anakabiliwa na suala la kutokomeza corona,” akasema Bw Dawood.

Bw Murungi ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la wabunge kutoka Meru, alisema hawatakubali kushiriki siasa wakati huu taifa liko pabaya kutokana na janga la corona na usalama wa kiafya wa raia wake.

“Viongozi wa chama chetu wanafaa kuonyesha uongozi mzuri na kuwajibikia Wakenya. Inasikitisha dunia nzima inaendelea kuhangaishwa na corona ilhali viongozi wetu wanashiriki siasa za chama,” akasema.