Siasa

Viongozi wa Kaskazini Mashariki wamtetea Duale

June 4th, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

VIONGOZI wa siasa kutoka Kaskazini Mashariki wamemtetea Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale mnamo kipindi ambapo mchakato wa kukusanya sahihi unaendelea kuwezesha kuondolewa kwake kama Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Hii ni baada ya Mbunge wa Kieni, Kanini Kega kuanzisha harakati hizo ambapo kufikia jana Jumatano alikuwa amekusanya sahihi 117 huku akilenga kufikisha 170.

Wakizungumza baada ya mkutano uliohudhuriwa na wabunge 12 kutoka eneo hilo, Seneta wa Garissa, Yusuf Haji amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kutogusa wadhifa huo wa Bw Duale wakati chama cha Jubilee – kwa kushirikiana na vyama washirika – kilifanya mabadiliko.

“Tunashukuru kwa nafasi iliyohifadhiwa ya Aden Duale kuendelea kuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa tangu mwaka 2013 hadi sasa. Tunataka kumhakikishia kiongozi wetu wa Jubilee kwamba viongozi kutoka Kaskazini Mashariki wamekuwa waaminifu kwa chama na yeye kama Rais,” amesema Bw Haji.

Naye Seneta wa Mandera Mahammed Mahamud amesema wamefurahia Duale kuendelea kuwa katika nafasi hiyo.

“Mwenzetu anastahili nafasi hiyo kwani amefanya kazi yake inavyostahili. Tunataka kumshukuru kiongozi wa chama chetu kwa kushikilia msimamo huo kwa watu wa Kaskazini Mashariki,” Bw Mahamud amesema.

Akaongeza: “Bw Duale ameongoza malengo ya chama na serikali vizuri bungeni.”

Seneta wa Wajir Abdullahi Ibrahim naye amewashajiisha viongozi wenzao wa kisiasa kufuata na kutii maneno ya Rais.

“Tunamuomba kiongozi wa chama atusamehe pale anahisi tumemkosea na tuko tayari kama viongozi wa Kaskazini Mashariki kuhakikisha kazi inafanyika jinsi atakavyo kiongozi wa nchi,” amesema Bw Ibrahim.

Duale aliponea kuangukiwa na shoka Jumanne chama cha Jubilee kilipotekeleza hatua ya kuwavua nyadhifa baadhi ya viongozi wanachama.

Duale ambaye amehudhuria mkutano wa viongozi wa eneo hilo awali alikuwa amesema kazi yake ni safi.

“Sikubahatika; kazi yangu ilionekana wazi. Hata hivyo, ni muhimu tutambue kwamba nafasi zinakuja na kwenda,” akasema Duale.

Walakini, wakosoaji wake wamedai kwamba bado yuko mashakani na siku zake zitatimia huku wakianza kukusanya sahihi za kuwezesha mchakato wa kuondolewa kwake.