Habari

Viongozi wa kidini wanitaka niirai serikali iruhusu maabadi kufunguliwa – Raila

May 22nd, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amefichua kwamba viongozi wa kidini wamemkimbilia aiombe serikali ifungue maabadi lakini akakataa kutokana na kuendelea kukithiri kwa virusi vya corona.

Maeneo ya ibada yalifungwa Machi baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya umma kutokana na janga la virusi vya corona nchini.

Bw Odinga amesema hakuweza kuridhia ombi la viongozi hao kwa sababu hakuwa na uhakika kuhusu njia ambayo makanisa yangehakikisha waumini wao wanazingatia maagizo ya kiafya yaliyotolewa na Wizara ya Afya kudhibiti idadi ya maambukizi.

“Viongozi wakuu wa kidini nchini walinifikia na kunitaka nitumie ushawishi wangu kurai serikali ifungue maabadi lakini nilikataa kwa sababu serikali italazimika kutumia maafisa wa polisi kuhakikisha raia wanadumisha hitaji la kukaa umbali wa mita moja na nusu,” akasema.

Ameongeza kwamba hana uhakika kwamba umefikia wakati wa kufungua maeneo ya ibada kwa sababu janga hili bado linaongezeka.

Baadhi ya viongozi wa kidini wamekuwa wakishinikiza serikali iyafungue maeneo hayo ya ibada wakidai kwamba maombi ni kati ya njia za kupigana na janga hili.

Aidha, Bw Odinga alitaka jamii ya Waluo kukomesha itikadi au tamaduni ya kusafirisha maiti hadi nyumbani na kuhudhuria matanga kama umati, akisema hiyo inahatarisha maisha yao wakati huu wa COVID-19.

Akizungumza katika kituo cha redio cha Ramogi FM, kiongozi huyo wa upinzani amesema amekasirishwa na wakazi wa Kibra hasa wale ambao waliandamana na msafara wa maiti hadi Siaya na baadaye wakapatikana wana virusi vya corona.

“Watu wa Kibra wamenikasirisha sana. Niliongea nao na wakabadilika lakini nimeshangaa baada ya serikali kuripoti kwamba watu wachache walipewa idhini na chifu kuandamana na msafara wa maiti. Wameambukiza wenzao; lazima tukomeshe tabia hii iwapo tuna nia ya kutokomeza corona

“Watu wetu wanafaa wakome kuhudhuria matanga kwa idadi yao. Waache wafu wazikwe na watu wachache na wanaoaga dunia jijini ni afadhali wazikwe Nairobi,” akaongeza Bw Odinga.

Virusi vya corona vimesababisha vifo vya watu 50 nchini.

Idadi jumla ya maambukizi kufikia Alhamisi ilikuwa visa 1,109 nchini Kenya.