Habari Mseto

Viongozi wa kidini washangaa vijana kulewa licha ya kulia kulemewa kiuchumi

January 3rd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi wa kidini na kijamii wameshangaa kwamba Wakenya wengi wanateta kuhusu gharama ya maisha kupanda lakini bado wako na pesa za kushiriki ‘dhambi’ za ulevi na mahaba kiholela.

“Huwaoni hata kanisani wakiomba Mungu na kupanda mbegu ili maisha wanayolalamika kuhusu yawape afueni. Lakini kwa ‘jaba’, pombe na mahaba wamefurika,” akasema Askofu Julius Mwaura akihubiri katika kanisa la Holy Ghost Terbanacle la Kigumo Desemba 31, 2023.

Alisema kwamba “tunafaa tuchunge kile kidogo tuko nacho na tuwekeze imani kwa Maulana kupitia sadaka na fungu la kumi”.

Askofu Mwaura alisema kwamba “kanisani utapata hata hatufiki 100 lakini baa zote wateja wengine wamesimama wengine hata wakiwa wameketi sakafuni wakiagiza kwa fujo pesa mkononi lakini sadaka inachunwa kwa mifuko kama kahawa”.

Akaongeza: “Hao ndio tena wanamlilia Mungu kwamba maisha ni magumu ndio awape afueni. Afueni gani ikiwa hata kile kidogo Mungu amewapa mnakimbia nacho kufupisha maisha yenu?”

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu katika ujumbe wake wa Krismasi alisema kwamba “kwa jumuia ya vijana tuko na shida kwa kuwa kunao wengi ambao sherehe ni pombe, bangi, Muguka na ngono”.

Bw Nyutu alisema kuna pesa za uchumi zinaelekezwa kwa masuala ambayo hayana manufaa yoyote kwa watumizi na uchumi kwa ujumla.

“Vijana wanatumia takribani zaidi ya Sh50 bilioni kwa mwaka katika sekta ya anasa. Kuna pesa zingine nyingi zinatumika katika sekta haramu na ambazo hatuwezi tukajumlisha kwa kuwa hakuna rekodi huwekwa na hata ushuru hauokotwi,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba baada ya matumizi hayo ya takribani Sh70 bilioni kwa mwaka, serikali hutumia zaidi ya Sh150 bilioni kila mwaka kukabiliana na athari za sekta hizo za ulevi, mihadarati na mahaba huku uchumi kwa ujumla kwa ukadriaji wa upana umepoteza takribani Sh1 trilioni.

[email protected]