Viongozi wa kidini wasuta wanasiasa kupepeta corona

Viongozi wa kidini wasuta wanasiasa kupepeta corona

Na Titus Ominde

VIONGOZI wa kidini Kaskazini mwa Rift Valley (North Rift) wameshutumu wanasiasa kwa kupepeta usambazaji wa virusi vya corona.

Mwenyekiti wa Baraza la Wahubiri na Maimamu (CIPK) kanda hiyo, Sheikh Abubakari Bini, alikemea wanasiasa hao kwa kutowajali Wakenya kutokana na mikusanyiko wanayoendelea kuandaa, akisema inawaweka wananchi katika hatari zaidi ya kuambukizwa corona.

Sheikh Bini alisikitika kuwa tabia hiyo ya wanasiasa inatishia kufunga nchi, na hususan kulemaza tena sekta ya elimu wakati huu wanafunzi wameanza mwaka mpya wa masomo.

Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret, mhubiri huyo alitoa wito kwa serikali kutowapendelea wanasiasa wanapokiuka masharti ya corona, na badala yake kuwachukulia hatua kali.

“Kuongezeka kwa Covid-19 nchi nzima kunasababishwa na kutokujali kwa wanasiasa ambao wahatarisha maisha ya Wakenya kupitia mikusanyiko yao na kupuuza itifaki zilizowekwa.”

Hisia zake ziliungwa mkono na mwenyekiti wa ushirika wa mchungaji wa Eldoret Re Bonifas Simani ambaye alisema wanasiasa wanapaswa kuongoza kwa mfano.

“Maagizo ya kupigana na Covid-19 hayapaswi kuelekezwa kwa Wakenya maskini pekee bali sisi sote lazima tuzingatie kanuni hizo bila kujali tabaka,” alisema kasisi Simani.

You can share this post!

Muturi awekewa presha aungane na Ruto, si Raila

Wakulima walalamikia kanuni mpya za miwa