Habari

Viongozi wa kidini wataka wanasiasa kuacha unafiki

October 11th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa kidini wamewahimiza wanasiasa nchini kuacha unafiki na kutubu kwa dhati ili kuepushia nchi maovu yanayoikumba kama ukabila, ufisadi na uongozi mbaya.

Wakihubiri wakati wa maombi ya kitaifa katika ikulu ya Nairobi, Jumamosi, viongozi hao walisema ni kwa kukubali makosa na kuyatubu kwa dhati na kusameheana ambako kutaunganisha Wakenya, kudumisha amani na kurejesha uthabiti wa kiuchumi na kijamii.

“Maombi ya toba yanafaa kuwa ya kweli. Hilo ndilo nchi inahitaji ili kuwa na uwiano,” alisema Askofu David Oginde wa kanisa la Christ For All Nations.

Maombi hayo yaliitishwa na Rais Uhuru Kenyatta kushukuru Mungu na kuombea nchi. Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali walisisitiza haja ya viongozi kuwa mfano mwema kwa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana kama njia moja ya kujenga jamii yenye amani na ustawi.

Walisema kwamba, Kenya inateseka kwa sababu ya viongozi kutotubu. “Fungueni macho yenu na muanze kuona. Kenya inaumia, Kenya inateseka. Mungu ahurumie nchi yetu,” alisema Askofu Martin Kivuva wa Dayosisi ya Mombasa ya Kanisa Katoliki.

Viongozi hao walisema toba na msamaha zitaleta amani, upendo na uthabiti nchini.

“Tunahitaji kujikumbuka sisi ni nani tunapokutana kama taifa mbele ya Mungu kuomba kama taifa,” aliongeza Askofu Sapit.

Maombi hayo yalifanyika wakati ambapo Rais Kenyatta na Naibu Wake William Ruto wametofautiana na kusababisha mgawanyiko katika chama tawala cha Jubilee.

Viongozi wa kisiasa huwa wanazungumza vyema wakiwa kwenye mikutano ya maombi lakini matamshi na vitendo vyao katika mikutano ya kisiasa huwa kinyume na vitendo vyao. Matamshi yao yamekuwa yakisababisha chuki na ghasia za kikabila maeneo tofauti.

Rais Kenyatta alisema aliitisha maombi hayo ili kushukuru Mungu kwa kusaidia Kenya kushinda changamoto nyingi.

Baada ya maombi hayo, Rais Kenyatta alisema amewasamehe wote ambao huenda walimkosea na akaomba wale ambao wanahisi aliwakosea wamsamehe pia.

“Tumeambiwa tusameheane na kwa hivyo ninataka kuomba msamaha kwa yeyote ambaye huenda nilimkosea. Ikiwa nilikosea mtu naomba anisamehe,” akasema Rais.

Akaongeza: “Ninachosisitiza na ambacho tumekumbushwa hapa ni amani, amani na umoja wetu kama taifa ndio furaha yangu kuu.”

Hakuna kiongozi mwengine wa kisiasa akiwemo Dkt Ruto ambaye alihudhuria hafla hiyo aliruhusiwa kuhutubu.