Viongozi wa kutoka Mlima Kenya wakutana Thika kuweka mikakati

Viongozi wa kutoka Mlima Kenya wakutana Thika kuweka mikakati

Na LAWRENCE ONGARO

VYAMA sita vya kisiasa vya viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya vilifanya kongamano mjini Thika, kwa minajili ya kujadili msimamo wao wa kisiasa katika siku zijazo.

Baadhi ya vyama hivyo ni Chama Cha Kazi cha Moses Kuria, Narc Kenya cha Martha Karua, na The Service Party (TSP) cha Mwangi Kiunjuri.

Vyama vingine ni New Democratic Party cha Dkt Thuo Mathenge, Peoples’ Party Of Kenya cha Jacob Gitau, na Democratic Party of Kenya cha Essau Kioni.

Kongamano hilo lililojumuisha viongozi zaidi ya 40 lilikuwa na madiwani wa zamani waliostaafu chini ya mwavuli wa Association Of Councillors, huku likiongozwa na Issac Kamunge.

Kulingana na kinara wa Narc Kenya Martha Karua ni kwamba kuna haja ya viongozi wa Mlima Kenya kuja pamoja na kujadiliana na kuzungumza kwa sauti moja.

“Kwa wakati huu, kila eneo la nchi, viongozi wa vyama tofauti wanafanya mikutano kwa minajili ya kupata mwelekeo mmoja hasa wakati huu tunapoelekea uchaguzini. Kwa hivyo, hata sisi kutoka Mlimani hatujaachwa nyuma,” alisema Bi Karua.

Alisema hakuna kiongozi yeyote kutoka Mlima Kenya ambaye amezuiwa kuingia katika mkutano huo.

Alisisitiza kwamba ni baada ya kuafikiana pamoja ndipo watajiandaa kwa kongamano kubwa Limuru 3 hivi karibuni.

Bw Mwangi Kiunjuri wa TSP alisema Mlima Kenya haitabagua na kwamba chama chochote kipo tayari kufanya mikutano ili wakifika kuzungumzia siasa za kitaifa watakuwa na sauti moja.

“Sisi kama wana Mlima Kenya, tunataka kuona ya kwamba tunazungumza pamoja ili tuamue kama jamii tutamuunga mkono kiongozi mmoja katika kinyang’anyiro cha kiti cha urais.

Bw Moses Kuria wa Chama Cha Kazi, alisema ni muhimu kwa Mlima Kenya kuungana kwa sababu hata maeneo mengine yanafanya hivyo ili kujipanga.

“Sisi pia kama jamii ya kutoka eneo la Kati hatutakubali kupangwa bali tutajipanga wenyewe ili kuamua mwelekeo ni upi wa kufuata,” alisema Bw Kuria.

Alisema kiongozi anayetaka kuongoza nchi ambaye atakubaliana na matakwa yao bila shaka watamuunga mkono.

Aliongeza kusema ya kwamba mikutano mingi Itaendelea kufanywa nchini ili kuafikiana kwa pamoja ni kiongozi yupi atakayefaa Wakenya kwa ujumla wao.

You can share this post!

OKA WAKAA NGUMU!

Yaya ashtakiwa kwa kuojesha mvulana wa bosi wake...