Habari MsetoSiasa

Viongozi wa ODM waasi Raila kuhusu suala la referenda

June 10th, 2019 1 min read

Na RUSHDIE OUDIA na LEONARD ONYANGO

BAADHI ya viongozi wa ODM wameenda kinyume na kinara wao Raila Odinga kuhusu pendekezo lake la kutaka kubuniwa kwa mfumo wa serikali tatu kwenye marekebisho ya Katiba.

Viongozi hao wakiongozwa na Gavana wa Kisumu Anyang Nyong’o na Seneta Moses Kajwang wa Homa Bay, wanasema itakuwa ghali mno kuendesha mfumo wa serikali tatu.

Bw Odinga amekuwa akipendekeza kuwepo kwa serikali 47 za kaunti, 14 za maeneo na moja ya kitaifa.

“Tunafaa kuangazia tena mfumo wa awali wa serikali za ugatuzi kama ilivyokuwa katika rasimu ya Katiba ya Bomas iliyopuuzwa. Rasimu ya Katiba ya Bomas iligawanya Kenya katika kanda 14. Mfumo wa serikali tatu utasaidia kumaliza changamoto zinazokabili serikali za kaunti,” akasema Bw Odinga alipokuwa akihutubia kongamano la tano la Ugatuzi lililofanyika Kakamega mwaka jana.

Serikali ya ngazi tatu inaungwa mkono na magavana wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho kwa lengo la kupata nafasi ya kuwania nyadhifa katika serikali za maeneo.

Lakini Gavana Nyong’o amepinga mfumo wa serikali ya ngazi tatu na badala yake anapendekeza kuwepo kwa mfumo wa bunge ambapo waziri mkuu atakuwa mkuu wa serikali.

Kulingana na Prof Nyong’o, tayari kaunti zimeungana kubuni miungano ya kiuchumi ya kimaeneo, hivyo hakuna haja ya kuleta mfumo wa serikali tatu.

“Kumekuwa na madai kwamba tunalenga kuweka serikali za ngazi tatu. Hiyo si kweli. Suala ambalo litaamuliwa na Wakenya ni ikiwa tutakuwa na mfumo wa bunge ambapo nchi inaongozwa na waziri mkuu au tuendelee na mfumo wa sasa,” akasema Seneta Kajwang.

Katika siku za majuzi viongozi wa ODM wameonekana kuchukua misimamo ambayo inakiuka kauli ya Bw Odinga, hali ambayo haikuwepo awali ambapo usemi wake ulikuwa wa mwisho na hakuna aliyethubutu kumpinga. Wakati sarafu mpya zilipozinduliwa, wakuu wa chama hicho walipinga hatua hiyo.