Habari Mseto

Viongozi wa Pwani walalama kuhusu unyakuzi ardhi ya umma

July 31st, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

VIONGOZI wa Mombasa wakiongozwa na Gavana Hassan Joho wamelalamikia unyakuzi mkubwa wa ardhi ya umma.

Aidha viongozi hao walisema ardhi ya umma inaendelea kunyemelewa na kunyakuliwa kiholelaholela.

Hata hivyo, viongozi hao walionya wanyakuzi hao dhidi ya vitendi hivyo huku wakiitaka tume ya ardhi nchini (NLC) na Wizara ya Ardhi kulinda mali ya umma na kutatua uovu huo.

“Tuna mipango ya kupanua soko zetu lakini mkiendelea kunyakua mashamba tutatekelezaje azma yetu? Yeyote anayedhania anaweza kunyakua mali ya umma anamzaha,” alisema Bw Joho kwenye uzinduzi wa soko la Shika Abadu wilayani Likoni Alhamisi.

Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko aliisihi serikali kulinda mali ya umma dhidi ya unyakuzi.

Kadhalika alimsihi gavana huyo kuendelea kutoa vyakula vya msaada kwa wakazi wake wanaoendelea kutaabika kutokana na janga la corona.

“Tunakupongeza kwa kuzindua for soko hili, lakini tunakusihi ishughulikie changamoto katika ufuo wa Shelly kama pale Jomo Kenyatta,” Bi Mboko.

Bi Mboko alimpongeza Bw Joho kwa kupigania haki za wapwani dhidi ya dhulma za kihistoria.

Bw Joho aliwasihi wakazi kuendelea kudumisha usafi ili kupigana na virusi vya corona.

“Tuendelee kuosha mikono na kuvaa barakoa ili kupigana na virusi hivi. Tutaendelea kupigana na virusi hivi,” akasema Bw Joho.