Habari Mseto

Viongozi wa Pwani wazomea waliounga Mswada wa Fedha

Na FATUMA BUGU June 23rd, 2024 2 min read

KIZAAZAA kilizuka katika kongamano la Jumuiya ya Kaunti za Pwani kujadili mkutano wao na Rais William Ruto hapo kesho (Jumatatu) kuhusu kuharamishwa kwa biashara ya muguka.

Mbunge wa Lamu Mashariki, Bi Ruweida Obo alizomwa na baadhi ya viongozi wenzake na hata kuitwa msaliti kwa kupigia kura kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

Hali hii ilichacha wakati Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana alipowashutumu baadhi ya viongozi wa Pwani kwa kuwa vigeugeu badala ya kuwa na msimamo.

“Kuna baadhi ya viongozi walisema hawatapigia kura kuupitisha Mswada wa Fedha lakini wakageuka kuwa vinyonga wakabadili msimamo wao bungeni,” alisema Gavana Godhana.

Matamshi hayo yalimkwaza Bi Obo ambaye alijitetea akisema atasimama na msimamo wake hata kura hizo zikipigwa tena Jumanne.

Hata hivyo, aliondoka kwenye mkutano huo huku akizomewa na kusimangwa na wabunge Mishi Mboko (Likoni), Bi Zamzam Mohammed (Mwakilishi wa wanawake Mombasa), mwenzake wa Kwale Bi Fatuma Masito.

Bi Mboko alimtaja kuwa msaliti na mtovu wa nidhamu kwa viongozi wenzake.

“Atoke aende hana heshima kwa Gavana Godhana kabisa!” Alisema Bi Mboko.

Mkutano huo ulikuwa wa kujiandaa kuwa na msimamo mmoja kabla kukutana na Rais William Ruto kujadili suala la biashara ya muguka wiki ijayo.

Kulingana na mwakilishi wa wanawake wa Kwale Fatuma Masito, haitakuwa rahisi kumshinikiza Rais kuunga mkono msimamo wao kwa hivyo viongozi wanafaa kujadiliana njia mwafaka za kutimiza malengo.

“Lazima viongozi tushirikiane na tuwe na msimamo mmoja, sio tuongee leo na kesho unahadaika,” alisema Bi Masito.

Msimamo wa viongozi hao wa Pwani aidha bado upo pale pale wakisema kuwa hawataruhusu ulaji wala biashara ya muguka katika kaunti za Pwani.

“Wakiendelea kuleta muguka kwa kutumia vichochoro itatulazimu na sisi tuchukue hatua kivyetu,” alisema Seneta wa Kilifi, Stewart Madzayo.

Bi Mishi Mboko alisema kuwa mkutano huo na Rais Ruto huenda usizae matunda kwani wanaokutana nao tayari wanapendelea upande mmoja.

Aidha, walisema hawatokubali kushinikizwa kubadili ajenda kuu ya mkutano huo na Rais William Ruto pindi watakapokutana naye. Baadhi yao walipendekeza kuwepo na maandiko ya ajenda hizo ili kuepuka kutoka nje ya mada wakati wa mkutano huo.

“Sisi kama magavana msimamo wetu ni ule ule, tusije tukafika kule wakaanza kusema tuzungumzie mambo na kudhibiti uuzaji na ulaji wa muguka kwani sisi hatutaki,” alisema Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir.