Habari MsetoSiasa

Viongozi wa Rift wasusia hafla ya Ruto, maswali yaibuka

October 1st, 2019 2 min read

BARNABAS BII na STANLEY KIMUGE

MASWALI yameibuka baada ya viongozi kadhaa katika eneo la Bonde la Ufa kukosa kufika katika hafla ya kuchangisha fedha iliyoongozwa na Naibu Rais William Ruto katika eneobunge la Kapseret, Uasin Gishu mnamo Jumapili.

Miongoni mwa viongozi waliosusia hafla hiyo ni Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago, Mwakilishi wa Wanawake Gladys Shollei, Seneta Margaret Kamar, wabunge Janet Sitienei (Turbo), Swarup Misra (Kesses) na Sila Tiren (Moiben).

Viongozi hao hawakueleza sababu zilizowafanya kukosa kuhudhuria hafla hiyo, licha ya kufanyika katika kaunti yao.

Mbali nao, viongozi wa Chama cha Jubilee (JP) katika kaunti jirani za Nandi na Elgeyo Marakwet pia hawakuwepo katika hafla hiyo.

Dkt Ruto anakabiliwa na upinzani mkali wa kisiasa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa jamii ya Wakalenjin, wanaoitaka jamii hiyo kufanya uamuzi huru kuhusu wa kuunga mkono kuwania urais mnamo 2022.

Kinyume na awali, ambapo amekuwa akikaribishwa na wabunge anapozuru eneo hilo, hali inaendelea kuwa tofauti kwani viongozi wengi wanaendelea kususia hafla zake.

Katika Kaunti ya Nandi, anakumbwa na upinzani baridi kutoka kwa viongozi mbalimbali kwa madai ya kumuunga mkono Gavana Stephen Sang licha ya tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Baadhi ya wabunge katika kaunti hiyo wanamtaka Bw Sang kujiuzulu.

Seneta Samson Cherargei wa Nandi na Mwakilishi Mwanamke Tecla Sum walikosa kuhudhuria hafla iliyohudhuriwa na Dkt Ruto mwezi uliopita, alikozindua mashine mpya za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kapsabet.

Juhudi za Dkt Ruto kuondoa tofauti kati ya Gavana Sang na Seneta Cherargei zimegonga mwamba, ambapo sasa anawataka wananchi kutowachagua viongozi wanaoendeleza siasa za migawanyiko.

Mwito huo haujapokelewa vizuri na wabunge wengi wa Jubilee.

“Ingawa tunamuunga mkono Dkt Ruto kuhusu masuala ya kitaifa, tunamwomba kuepuka kuingilia siasa za eneo hili kwani anaegemea upande wa baadhi ya viongozi,” akasema mbunge ambaye hakutaka kutajwa.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wabunge wengine wa chama hicho, walioshangaa mbona Dkt Ruto amekuwa akizindua upya miradi inayoendeshwa na serikali ya kitaifa ili kunda taswira kuwa serikali ya kaunti inafanya kazi.

“Haina manufaa kuhudhuria hafla za Dkt Ruto, ambapo baadaye utadharauliwa na gavana ambaye anataka kuonekana kuwa ndiye anayefanya kazi licha ya miradi mingi kuendeshwa na serikali ya kitaifa.

Dkt Ruto anapaswa kutuacha kukabiliana sisi wenyewe kwa wenyewe,” akasema mbunge mwingine ambaye hakutaka kutajwa.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Dkt Ruto anapaswa kuangazia masuala ya maendeleo na kukoma kuingilia siasa za kikanda.

“Kwa sasa, kila mwanasiasa anapanga kuhusu mustakabali wake. Dkt Ruto anapaswa kuendelea kuangazia masuala ya maendeleo kote nchini,” akasema Bw Philip Chebunet, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

Dkt Ruto anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya viongozi waliokuwa wakimuunga mkono.

Baadhi yao wamehamia vyama vya Kanu na Chama Cha Mashinani (CCM) vinavyoongozwa na Seneta Gideon Moi (Baringo) na aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto mtawalia.

Bw Moi amekuwa akikutana na viongozi wa kisiasa na watu maarufu ili kuimarisha uungwaji mkono wake wa kisiasa katika eneo hilo, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto.