Kimataifa

Viongozi wa serikali mpya wamtembelea Bashir jela

September 2nd, 2019 2 min read

NA AFP

VIONGOZI wa Baraza jumuishi la uongozi nchini Sudan, jana walimtembelea aliyekuwa Rais Omar al-Bashir katika gereza maarufu la Kobar, Kaskazini mwa Khartoum anakoendelea kuzuiliwa baada ya kuondolewa mamlakani mwezi Aprili mwaka huu.

Kiongozi wa baraza hilo Aisha Mousa na ujumbe wake walimtembelea Bashir pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa kama njia ya kuthibitishia raia wa Sudan kwamba viongozi hao wa utawala uliopita bado wapo kizuizini.

Kulingana na taarifa rasmi kutoka kwa Mousa, viongozi 23 ambao walikuwa kwenye serikali ya Bashir wanaendelea kuzuiliwa wakingoja kuhukumiwa kwa makosa mbalimbali.

Mousa pia alifichua kwamba ujumbe huo uliandaa mazungumzo ya kina na Bashir na kumhakikishia kwamba mchakato wa kupata haki hautaingiliwa kivyovyote kisiasa.

Wakati uo huo, mawaziri wa kuhudumu kwenye baraza hilo wanatarajiwa kutajwa wiki hii.

Duru ndani ya baraza hilo zilieleza kwamba mashauriano kuhusu viongozi wa kuteuliwa kuhudumu kwenye serikali yamekamilika na kilichosalia ni kutangazwa pekee.

Habari hizo zilifafanua kwamba orodha ya majina ya mawaziri iliyowasilishwwa na Chama cha Upinzani (FCA) kwa Baraza la Mpito la Jeshi(TMC) iliidhinishwa na hakuna jina lolote lililokataliwa.

Vilevile mkutano kati ya maafisa wa FCA pamoja na Waziri Mkuu Abdalla Hamdok jana ulifanyika lengo kuu ikiwa kuorodhesha wasifu wa mawaziri wapya kabla ya kuyatangaza majina yao rasmi.

Serikali itakayoongozwa na Hamdok itawajumuisha mawaziri 19 na wanachama watano wa mabaraza makuu.

Baraza jipya la mawaziri lilitarajiwa lizinduliwe Jumamosi na kuapishwa Jumapili lakini kukaibuka tofauti chache ambazo zilichangia tangazo hilo kutotolewa kabla ya makataa ya Agosti 31.

Ziara ya Mousa na kundi lake lilijiri siku moja tu baada ya Bashir kushtakiwa kwa kutumia na kupata fedha za kigeni kwa njia ya haramu, makosa ambayo huenda yakamvutia kifungo cha miaka 10.

Akiwa mbele ya mahakama kwa kikao cha tatu cha kusikiza kesi yake, Jaji Al-Sadiq Abdelrahman aliorodhesha mashtaka matatu yanayomkabili Bashir.

“Maafisa wa usalama wa serikali walipata Sh2.5 bilioni nyumbani kwako ambazo ulipokea na kutumia kwa njia zisizofaa,” akasema Jaji Abdelrahman.

Hata hivyo, Bashir alijitetea na kueleza korti kwamba alipokea pesa hizo kutoka Mwanamfalme wa Saudia Mohamed bin Salman huku wafuasi wake na jamaa zake wakiimba ‘Allahu Akbar’ kama njia ya kumtia moyo.