Habari Mseto

Viongozi wa UDA Pwani wajongea vita dhidi ya muguka

June 3rd, 2024 2 min read

NA SIAGO CECE

VIONGOZI wa Pwani wameweka kando tofauti zao za kisiasa ili kupambana dhidi ya athari za miraa na muguka.

Licha ya Rais William Ruto kuonyesha na ya kusaidia ukuzaji zaidi wa mmea huo, wanasiasa wa chama chake cha UDA katika eneo la Pwani wanashikilia msimamo wa kuweka sheria kali dhidi ya matumizi ya bidhaa hizo.

Wanasiasa hao sasa wanashinikiza mageuzi ya sheria kuhusu ili miraa na muguka zitambuliwe kama mihadarati badala ya mimea ya kilimo.

Akizungumza huko Ukunda, Mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader, alisema pendekezo lililowasilishwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, litalenga kubadilisha sheria.

Bw Bader alisema wabunge wa Pwani watawashawishi wenzao kutoka maeneo mengine ili kuhakikiha mswada huo umepitishwa.

“Mashirika ya serikali pia yanafaa kufanya utafiti wa Muguka na Miraa ili sote tuielewe na kujua jinsi ya kuitumia kama dawa nyingine,” Bw Bader alisema.

Kwa upande wake, Bw Baya, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Wengi bungeni alisema atapambana na muguka bungeni, kwani tayari amewasilisha notisi kwa Spika wa Bunge la Taifa kutaka kuwasilisha Mswada wa kurekebisha Sheria ya Mazao ya 2022.

“Wananchi walinipa jukwaa na nitatumia kufanya shughuli zangu kwa niaba ya wananchi. Hapo ndipo sheria ilipotungwa na ndipo itafanyiwa marekebisho. Hapo ndipo nitakwenda kupigana na watu wangu,” alisema.

Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, ambaye pia ni mwanachama wa UDA, amepongeza hatua ya wabunge akisema kuwa itachukua jukumu muhimu katika kudhibiti matumizi ya muguka na miraa.

“Ninataka kumshukuru Owen Baya ambaye amewasilisha hoja yake kwa bunge. Kwa sababu makosa yalifanywa na Bunge kwa kuainisha muguka kama zao la biashara na sio kama dawa za kulevya,” Bi Achani alisema.

Aliongeza kuwa kwa vile sheria bado inahalalisha mmea huo hatari, serikali ya kaunti na bunge wanajitahidi kudhibiti matumizi yake huko Kwale kupitia hatua kali.

“Tunataka kuhakikisha kuwa muguka hatapatikana kwa mtu yeyote wa kawaida katika kaunti. Kiasi ambacho tumeweka kwa magari yanayoingia Kwale kitahakikisha kuwa bei ya bidhaa hizo imeongezwa,” alisema.

Katika sharia mpya, malori ya muguka inayoingia Kwale kaunti itahitajika kulipa Sh300,000 katika vituo vya malipo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, pia alitangaza msimamo wa kuunga mkono marufuku dhidi ya muguka Kilifi.

Hata hivyo viongozi wa kidini wamepuulizia mbali hatua ya gavana huyo kuongeza ushuru wa bidhaa hiyo wakisema haitasaidia kudhibiti biashara ya muguka.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kwale Muslim Development Initiative (KMDI) Sheikh Mwakidudu Sauti, wamemtaka Bi Achani aweke mbinu kali zaidi ya kuepukana na majanga yanayosababishwa na muguka hasa kwa vijana.