Habari

Viongozi wa vyama kadhaa nchini Kenya waendelea kubamizwa ukutani

June 9th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BAADHI ya wanachama wa Amani National Congress, ANC, wameanza kuitisha uchaguzi mpya wa uongozi wa chama hicho.

Bw Musalia Mudavadi ndiye kiongozi wa chama hicho kwa sasa.

Mbunge maalum Godfrey Osotsi, amesema Jumanne  muda wa uongozi wa sasa wa ANC unakamalika Jumatatu, Juni 15, 2020, na kwamba umewadia wakati wa kubadilisha viongozi walioko.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, Osotsi amesema kukamilika kwa muda wa uongozi wa sasa kunakaribisha fursa ya kusafisha chama.

“Huu ndio wakati wa kusafisha vyama vinavyoongozwa na watu wenye tamaa ya ubinafsi. Kwa sababu ya matakwa ya wananchi na wanachama, ninaagiza uchaguzi mpya ANC ufanyike tubadilishe viongozi,” mbunge huyo maalum amesema.

Akaongeza: “Kuanzia Jumatatu, Juni 15, 2020, tutaanza harakati za kuitisha uchaguzi wa ANC.  Sharti ifahamike kwamba hakuna atakayetimua Musalia Mudavadi kwa njia isiyo ya kidemokrasia.”

Bw Osotsi amepinga madai kuwa yeye ni kibaraka wa Raila Odinga (ODM) na kwamba anapanga njama ya kubadilisha uongozi wa ANC kisiri.

Badala yake amesema viongozi walioko “walianza kujitimua wenyewe chamani mwaka 2018 walipopinga handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 9, 2018.

Mbunge huyo maalum akionekana kutetea Raila kufuatia msukosuko unaoshuhudiwa ANC, alisema kwa vyovyote vile kiongozi huyo wa ODM hahusishwi na masaibu yaliyoibuka.

“Mimi si mwanachama wa ODM, lakini tuache kuingiza Raila Odinga katika shida zetu wenyewe na tulizojitafutia. Ninaambia ndugu zetu, ikiwa wanataka kujiunga na Naibu Rais William Ruto, kuna njia nyingi. Waache kutafuta vijisababu. Safari ya Musalia kuungana na Ruto ilianza alipopinga Handisheki,” Osotsi akasema.

Amedai kuwa kuna baadhi ya wanachama wa ANC wanatembelea Dkt Ruto kisiri kufanikisha muungano kati yake na Bw Mudavadi.

Msukosuko wa ANC umeanza kushuhudiwa siku chache baada ya ule wa Ford-Kenya ambapo Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alibanduliwa.

Baadhi ya wanachama wa Ford-Kenya walimteua Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi kama kiongozi.

Msajili wa vyama vya kisiasa nchini Anne Nderitu alichapisha mabadiliko hayo katika Gazeti Rasmi la Serikali, ingawa seneta Wetang’ula ameendelea kuyapinga.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amekuwa akinyooshewa kidole cha lawama kwa masaibu yanayozingira Ford-Kenya pamoja na ya chama tawala cha Jubilee.