Viongozi waelezea matumaini ya uchaguzi wa amani

Viongozi waelezea matumaini ya uchaguzi wa amani

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI wa kidini Rift Valley wanatumai kuwepo uchaguzi wa amani katika eneo hilo licha ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuorodhesha eneo hilo miongoni mwa yanayoweza kushuhudia ghasia za baada ya uchaguzi.

Wakizungumza katika hafla ya staftahi na maombi kwa dini mbalimbali katika hoteli ya Starbuck, walisema kufuatia mfululizo wa kampeni na maombi ya amani katika eneo hilo, wanaamini hakutakuwa na ghasia za aina yoyote baada ya uchaguzi.

Askofu Dominic Kimengich wa kanisa la Katoliki dayosisi ya Eldoret alitoa wito kwa wakazi kudumisha amani hata baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Kama makasisi tumeridhishwa na hatua zilizowekwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani. Tunatoa wito kwa washikadau wote kushirikiana na vyombo vya usalama vya serikali ili kuhakikisha mazingira ya amani katika kipindi hiki,” alisema askofu Kimengich.

Askofu Kimengich aliwataka wakazi wa Kerio Valley ambao wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa usalama kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao kwa njia ya kidemokrasia na amani bila uoga.

Alisema kuwa kwa sasa kuna utulivu katika eneo la Kerior Valley kwa hivyo wakazi hawana cha kuogopa ila kujitokeza kwa wingi na kuwapigia kura viongozi wao.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aahidi wakazi ushindi mkuu

Mamilioni ya Wakenya washiriki uchaguzi leo

T L