Habari Mseto

Viongozi wahimizwa kuchapa kazi

November 23rd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wamehimizwa kuzingatia ajenda nne muhimu za serikali badala ya kujihusisha sana na siasa za mwaka wa 2022.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni Wa Muchomba, amewataka viongozi wote wajihusishe na kuchapa kazi ili kufanikisha ajenda nne kuu za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Na ni kwa msingi huo ambapo alimsihi Rais aanze kuchukua hatua dhidi ya waziri yeyote asiyefuata mwelekeo unaostahili kuhusu ajenda nne za serikali.

“Ni jambo la kushangaza sana kuona mawaziri wachache waliopewa majukumu ya kufanyia Wakenya kazi wanapoteza muda wao mwingi wakiangazia siasa za 2022. Mawaziri kama hao wanastahili kupigwa kalamu mara moja bila kupoteza muda,” alisema Bi Wa Muchomba.

Alitoa mfano wa fedha Sh2 bilioni za Coffee Cherry Advance Fund, zilizotolewa kwa wakulima wa kahawa miezi 18 iliyopita lakini hadi wa leo bado wakulima hao wanangoja fedha hizo.

Alitaka kiongozi wa nchi kumulika kwa makini Wizara ya Kilimo na ile ya Biashara ambazo alisema zinaonekana haziwajibiki ipasavyo.

“Iwapo wale wamepewa majukumu kuzisimamia wizara hizo hawawezi wakafanya kazi ipasavyo, basi wajiuzulu na kuachia wale wanaostahili waendeshe kazi hizo,” alisema Bi Wa Muchomba.

Alisema viongozi kama kweli wana hamu ya kuonyesha utendakazi wao basi ni wakati huu lakini sio kuhadaa wananchi na siasa za 2022.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa mjini Thika wakati wa hafla ambapo vijana wapatao 1000 kutoka Kaunti ya Kiambu walionyesha vipaji vya katika mashindano yaliyopewa jina ‘Youth Talent Show’.

Kujitegemea

Aliwahimiza vijana kuwajibika kwa kukuza talanta zao ili kuwa na maisha ya kujitegemea hapo baadaye.

Waziri wa Vijana na Jinsia Prof Margaret Kobia, alisema serikali inahimiza vijana kukuza talanta zao huku wakishauriwa kujiepusha na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe ambayo ni hatari si tu kwa afya zao bali pia kwa mfumo wao wa maamuzi muhimu.

“Nyinyi vijana mnayo nafasi ya kujiendeleza katika siku za usoni na kwa hivyo sio vyema kuharibu maisha yako bure. Ni vyema kuwa na maadili mema na kujiamini katika maisha,” alisema Prof Kobia.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh100 milioni ambazo kusudio ni ziweze kunufaisha vijana kuendesha biashara na talanta zao.

“Nyinyi vijana mlio hapa ni vyema kutambua ni jambo lipi mnalostahili kufanya katika maisha ili muweze kujiendeleza. Huu sio wakati wa kuharibu maisha kwa kuchukua hatua zisizo za busara,” alisema waziri huyo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Filamu na Uainishaji nchini Kenya (KFCB) Ezekiel Mutua, aliwashauri wazazi wawe makini kufuatilia mienendo ya wana wao hasa wakati huu wa likizo ndefu.

“Ninatoa mwito kwa wazazi popote walipo wafanye hima kuona ya kwamba wanafuatilia kwa makini ni vipindi vipi wana wao wanatazama wakati huu wanapokuwa likizoni,” alisema Mutua.

Alisema wakati huu wazazi wana kibarua kikubwa kuona ya kwamba wanafuatilia miendendo ya watoto wao na kuwashauri jinsi ya kupatana na vijana wenzao kwa kuwajulisha wachague vikundi wanavyojumuika navyo.

Alisema kwa siku za hivi karibuni “tumesikia kwenye habari vijana wengi wakijinyonga na maswala ya ubakaji, na haya yote yanatokana na ukosefu wa maadili mema katika jamii.”

Katibu katika wizara ya habari na teknolojia Bw Gerom Ochieng’ alisisitiza umuhimu wa kuzingatia teknolojia kwa sababu huo ndiyo mwelekeo ambao dunia nzima inaufuata kwa sasa.

“Vijana wana nafasi kubwa ya kukumbatia teknolojia ya ICT kwa sababu kila mahali sasa ni hiyo teknolojia inazingatiwa. Kwa hivyo, ni vyema wawe makini kwa kuzingatia mwelekeo huo,” alisema Bw Ochieng’.