Habari Mseto

Viongozi wahimizwa wamche Mungu na wawatumikie wananchi

January 17th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI nchini wamehimizwa kuzingatia maendeleo na kutendea wananchi kazi badala ya siasa za kila mara.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliwashauri wananchi kuwachagua viongozi wenye maono ambao wanawajali kwa kuleta maendeleo na kuwatumikia kwa uwazi.

“Nchi hii mahali imefika sasa inataka wananchi wajisahili na wachague viongozi waliowajibika na walio na maono ya kufanikisha maisha ya wananchi,” alisema Bw Wainaina.

Alisema viongozi wengi wanapenda kupumbaza wananchi kila mara bila kuwa na ajenda yoyote ya maendeleo mawazoni mwao.

Aliyasema hayo manamo Alhamisi wakati wa maombi rasmi ya kufungua mwaka yaliyofanyika kwenye afisi yake ya NG-CDF mjini Thika.

Alitoa mfano wa nchi ya Rwanda ambayo alisema imeinuliwa kiuchumi na Rais Paul Kagame kwa kuwateua mawaziri wenye maono na uwajibikaji.

“Nchi hii ina utajiri mwingi ajabu ambapo ikiwa kila kiongozi na mwananchi anaweza akafanya uamuzi wa kuwajibika katika kila jambo, bila shaka tutatambulika kama nchi iliyopiga hatua kimataifa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema eneo lake la Thika lilitajwa kama lilotumia fedha zake za maendeleo kwa uwajibikaji na uwazi.

Alitoa mfano na kueleza ya kwamba kwa fedha za maendeleo alizopokea mwaka wa 2019, Sh 48 milioni ziliweza kukarabati shule 30 za msingi zilizokuwa katika hali mbovu.

Askofu mkuu wa kanisa la Evanjelisti la Christian Church International (CCI), Bw Henry Mulandi, alikishauri kizazi cha sasa kuwa makini na kufuata mienendo ya wazee wao.

Kuwatumikia wananchi

Aliwahimiza viongozi popote walipo kupunguza joto la siasa linaloshuhudiwa kwa wakati huu nchini na kujihusisha na kutumikia wananchi.

“Wakati huu sio wakati wa kupiga siasa lakini ni vyema kuona ya kwamba majukumu waliyopewa na wananchi yanatekelezwa vilivyo,” alisema Askofu Mulandi.

“Siku hizi vijana wamejawa na tamaa nyingi kiasi kwamba wanaabudu vitu vya dunia kuliko kumcha Mungu,” alisema askofu Mulandi.

Aliwahimiza pia wazee kuwapa wosia wana wao ili nao waweze kuelewa hali ya maisha ya baadaye ni ipi.

Aliwataka viongozi kuachana na siasa za kila mara na kuzingatia maendeleo.

“Kwa wakati huu siasa za nchi yetu zimechacha kweli ambapo wananchi wameachwa pweke wasijue la kufanya,” alisema mchungaji huyo.

Aliwataka wananchi wamrudie Mwenyezi Mungu ili waweze kupata mwelekeo mwema.