Habari Mseto

Viongozi waitaka serikali kuwakumba vijana kwa kuwaajiri

June 26th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wamependekeza maslahi yao yazingatiwe na serikali wakati inaajiri watu.

Seneta maalumu Bw Isaac Mwaura, alisema Jumanne kwa muda mrefu vijana wamewekwa kando inapofika wakati ajira zinapoendeshwa serikalini.

Kwenye kongamano hilo la vijana lililofanyika mjini Ruiru na ambalo lilihudhuriwa na vijana zaidi ya 200 walijadiliana kwa uwazi masaibu wanayopitia baada ya kukamilisha elimu yao katika viwango mbalimbali.

Bw Gedion Keter, ambaye ni mbunge maalumu naye alisema cha muhimu ni vijana kuhamasishwa kuhusu haki zao.

“Ninawahimiza vijana mjitokeze wazi ili muweze kutambulika. Ili kufanikiwa, ni sharti ujitambulishe kwa umma,” alisema Bw Keter.

Alipendekeza vijana waajiriwe kwa wingi kusimamia na kufanya sensa.

“Si vyema kuajiri watumishi wa serikali katika shughuli hiyo wakati vijana wengi wenye ujuzi hawana ajira,” alisema Keter.

Bi Florence Mukami naye kwenye kongamano hilo alisema vijana wanastahili kushirikiana pamoja ili kutatua shida zao.

“Vijana wanastahili kuinuliwa kwa kupewa ajira badala ya kuajiri wazee. Mara nyingi wazee ndio hupata nafasi za ajira,” alisema Bi Mukami.

Vijana washauriwa kujiamini

Bw Cyrus Omondi, Diwani wa Kahawa Wendani aliwashauri vijana kujiamini kwa kujitokeza wazi ili kuonyesha ujuzi wao.

“Vijana mnastahili kuwa mstari wa Mbele kuonyesha kuwa mnao uwezo wa kujisimamia,” alisema Bw Omondi.

Kuhusu siasa za nchi Bw Isaac Mwaura alisema chama cha Jubilee kinastahili kuweka nyumba yake imara.

“Ni muda mrefu viongozi wa chama cha Jubilee hawajafanya mkutano wowote kujadili maswala mazito yanayokikumba. Hata sisi tulio chamani tumeshindwa kuelewa kwa nini hakuna majadiliano,” alisema Bw Mwaura.

Aliwashauri viongozi wa Mlima Kenya kuzungumza kwa sauti moja la sivyo watajilaumu wenyewe wakigawanyika.

Seneta maalumu Bw Isaac Mwaura ahutubia waandishi wa habari mjini Ruiru,baada ya kongamano la vijana. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwataka viongozi wanaozunguka kote nchini wasitishe mipango yao na badala yake wazingatie maendeleo kwa miaka mitatu ijayo.

Mbunge wa Molo Bw Kuria Kimani alisema viongozi wa Mlima Kenya hawatakubali kutengwa kwa migawanyiko.

“Tunataka kuona chama cha Jubilee kikiendesha mambo yake kwa mwongozo mmoja bila migawanyiko. Sisi kama viongozi tusikubali kugawanywa kwa misingi ya vyama,” alisema Bw Kimani.

Aliwashauri viongozi kuzingatia maendeleo ya serikali badala ya kuibua taharuki kwa kuingizia Wakenya wasiwasi.