Habari Mseto

Viongozi wajuta kumuunga mkono Raila uchaguzini

April 4th, 2018 1 min read

Na GERALD BWISA

VIONGOZI wa Ford Kenya kutoka Kaunti ya Trans Nzoia Jumanne walieleza majuto yao kwa kumuunga mkono Kinara wa ODM, Raila Odinga kwenye chaguzi za 2013 na 2017.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kwanza, Bw Ferdinand Wanyonyi, viongozi hao walikashifu kuvuliwa majuzi kwa kiongozi wao Moses Wetang’ula wadhifa wake wa kiongozi wa wachache katika Seneti.

“Tumejifunza kutokana na usaliti wa ODM na Raila atakuwa na kibarua kigumu kupata uungwaji mkono kutoka eneo hili siku zijazo,” akasema Bw Wanyonyi alipohutubia wanahabari mjini kitale.

Naye Diwani wa Motosiet, Bernard Muganda alisema watabuni mbinu ya kushirikiana na viongozi kutoka maeneo mengine na kuwataka wafuasi wao kutokata tamaa.

“Si lazima tushirikiane na watu kutoka Nyanza. Tunaweza kuunda miungano na watu kutoka maeneo mengine kama Bonde la Ufa na Kati,” akasema.

Bw Wanyonyi alisema mkutano walioandaa majuzi na Naibu Rais haimanishi wameanzisha ushirikiano wa kisiasai.