Habari MsetoSiasa

Viongozi wamwomboleza Jonathan Moi

April 21st, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na FRANCIS MUREITHI

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, Jumamosi waliwaongoza viongozi wengine wakuu nchini kuomboleza kifo cha mwanawe Rais mstaafu Daniel Moi, Jonathan Toroitich.

“Namwomba Mungu awape neema na nguvu kustahimili msiba huo mkubwa,” Rais Kenyatta akamwambia Mzee Moi.

Alisema Jonathan aliyepata umaarufu katika miaka ya 80 kwa kushiriki katika mashindano ya magari ya Safari Rally, alikuwa mtu mpole, mkarimu na jasiri pamoja na kuwa mtu wa kutegemewa.

Rais mstaafu Mwai Kibaki alimtaja marehemu kama mtu aliyebobea katika maswala ya biashara na uwekezaji.

“Nakumbuka familia ya Mzee Daniel Arap Moi kwa maombi wakati huu wa msiba,” akasema kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari na msemaji wake Ngari Gituku.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka pia walitoa rambirambi zao.

Kwenye jumbe walizotuma kwa vyombo vya habari na pia kupitia mitandao ya Twitter, viongozi hao wawili waliofanya kazi na Mzee Moi, walimpa pole kwa kifo hicho.

Msemaji wa Mzee Moi, Bw Lee Njiru alisema Jonathan alifariki Ijumaa jioni mjini Nakuru.

“Nimeagizwa na familia ya Moi niwajulishe Wakenya kuhusu kifo cha mwanawe Jonathan Moi. Wapatieni nafasi waomboleze mpendwa wao kwa upole,” akasema Bw Njiru.

Rais mstaafu Moi ana watoto wanane, watano wa kiume na watatu wa kike. Wao ni Gideon, Philip Moi (mwanajeshi mstaafu) na dadake pacha Doris Elizabeth Chepkorir, Jennifer, June, Raymond Moi ambaye ni Mbunge wa Rongai na John Mark.

Mama yao Lena Moi alifariki mnamo 200.