Habari Mseto

Viongozi wanawake kuomboleza hadharani mauti ya misukosuko ya ndoa na uchumba

May 30th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WABUNGE wanawake katika Seneti, Kaunti na bunge la kitaifa kwa ushirikiano na wadau wengine wa kutetea haki za wanawake Ijumaa wamepanga kushiriki maombolezo ya hadhara katika Freedom Corner, Uhuru Park jijini Nairobi.

Kundi hilo ambalo linajifahamisha kama Embrace na ambalo liliundwa mwaka 2018 hujumuisha wabunge wote wa kike hapa nchini na ambao huandamana mashinani kwa kuonyesha umoja wao bila kujali misingi ya chama, kabila na siasa kuunganisha Wakenya.

Kundi hilo lilikuja pamoja baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kuridhiana na kuamua kuunganisha Wakenya, viongozi wa kike wakikumbatia harakati hizo kwa kuunda muungano huo wao, viongozi wa kiume wakizembea kuunda mrengo wao rasmi.

Maombolezo hayo yatakuwa ya kuwakumbuka wanawake ambao wameuawa katika ndoa au uchumba hapa nchini.

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo la wanawake ambalo kwa pamoja huhubiri amani katika jamii, Naomi Shaban, watakongamana katika bustani hiyo kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa tatu na ambapo kilele kitakuwa maandamano ya amani ya muda mfupi.

Alisema kuwa mavazi ya kushiriki hafla hiyo yatakuwa meupe na ambapo michumaa itawakishwa katika bustani hilo kama kilele cha maombolezi hayo.

“Tutakuwa hapo kusimama na wanawake ambao wameaga dunia mikononi mwa ukatili wa kimapenzi na ndoa,” Bi Shaban aliambia Taifa Leo.

Alisema kuwa ujumbe wa siku utakuwa wa kuwataka wanaume wakichoshwa na uhusiano walio nao na wachumba wao wa kike au wake zao, wawe tu wakiwanusuru wanawake hao mauti.

Ni hali ambayo inaangazia wanaume kukosa ule umoja wa kushughulikia wenzao ambao pia wameangamia katika misukosuko hiyo ya kimapenzi na ndoa ikizingatiwa kuwa jinamizi hili limekuwa na mazoea ya kukata mbele na nyuma kama msumeno.

Wengi huenda wabakie wakijiuliza kile chama cha Maendeleo ya Wanaume cghake Nderitu Njoka kilienda wapi na mbona hakina mikakati sawa na hii ya wanawake, huku ripoti zikizidi kuibuka kuwa wanaume siku hizi pia ni waathiriwa wa vita katika ndoa mikononi mwa wake zao.

Spika wa bunge la Kitaifa, Justin Muturi aliambia Taifa Leo “kwa hili sina usemi kamwe kwa kuwa ni hafla nje ya bunge.”

“Niko tu na usemi wa udhibiti wakati wabunge hawa wako katika bunge wakishiriki kazi yao rasmi. Kwa hili la wabunge wa kike kuandamana na wenzao wengine kuomboleza hadharani sina usemi kamwe. Kile ninajua ni kuwa hata wanaume hawajafungiwa nje kushiriki hafla sawa au wajiunge na wanawake hawa katika harakati hizi. Ni suala la maamuzi yao,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa kunafaa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu suala hili la misukosuko ya ndoa na hali ya wengi kuamua kutekeleza ukatili dhidi ya wenzao na wengine kujiua.

“Sio sawa kamwe, kuna shida kubwa na ni janga letu kama jamii na ambalo tunafaa kulivalia njuga tukisaka suluhu. Ni suala la wadau kuja pamoja kusaka hiyo suluhu. Lakini sio kusema hawa wanawake hawajafanya uamuzi wa busara; labda hata wanaume nao wanajipanga na tutawaona wakizingatia jinamizi hili kulipa suluhu,” akasema.