HabariSiasa

Viongozi wataka Joho awanie urais 2022

February 17th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

BAADHI ya viongozi wa kisiasa kutoka Pwani jana walimtaka gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwania Urais mwaka wa 2022.

Walikuwa wakiongea katika ukumbi wa mikutano wa Mikindani Kwa Shee Jumamosi baada ya kuanzishwa rasmi kwa kituo cha kukuza talanta kwa vijana wa Jomvu.

Viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Jomvu, Bw Badi Twalib walisema kuwa gavana Joho anatosha kuendesha nchi hii akipatiwa nafasi.

Akiwemo Seneta wa Mombasa Mohamed Faki, spika wa bunge la Mombasa Arub Khatri na wawakilishi kadha wa wadi viongozi hao walisema wataunga mkono juhudi za Bw Joho kuwania Urais.

“Kutokana na yale ambayo umefanya kote Pwani ikiwemo kutuunganisha pamoja, wewe kwa sasa ndiye tunayekutizama kama Rais mwaka wa 2022. Hatuna mwengine kwa sasa,” akasema Bw Twalib.

Mbunge huyo alisema kuwa watasukuma gavana huyo kuwania urais ili shida zinazowakumba watu wa Pwani zishughulikiwe kwa kina.

“Tuko na rekodi yako ya maendeleo kama Wapwani kwa hivyo hatuna shaka lolote tunaposema kwamba tunataka uwe Rais. Tunajua ukiwa pale, zile shida ambazo tunakumbana nazo Pwani zitaisha,” akasema mbunge huyo.

Hata hivyo, gavana Joho alikwepa kulizungumzia swala hilo aliposimama kuhutubu.

Badala yake alilalama kuhusu mashirika ya umma ambayo alisema yanabagua makabila mengine wakati wa kuajiri wafanyakazi.