Viongozi wataka kaunti  8 za Mashariki kuungana

Viongozi wataka kaunti 8 za Mashariki kuungana

Na MWANDISHI WETU

BAADHI ya wanasiasa kutoka kaunti nane za uliokuwa mkoa wa mashariki Kenya wanataka eneo hilo kuungana kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakiongozwa na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na mwenzake wa Machakos Alfred Mutua, viongozi hao wanasema kwamba kuungana kwa eneo hilo kisiasa kutawapa wakazi nafasi ya kutetea maslahi yao katika serikali ya kitaifa.

Mkoa wa Mashariki uliohusisha kaunti kaunti za Meru, Marsabit, Isiolo, Embu, Machakos, Kitui Makueni na Tharaka Nithi ambayo ilibuniwa chini ya mfumo wa utawala wa ugatuzi.

Wakizungumza Ijumaa katika eneo la Kiagu, Imenti ya Kati kaunti ya Meru, magavana hao walisema kwamba vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi eneo hilo vinapaswa kuungana ili liwe na nguvu kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Tunahitaji muungano mkubwa ambao utaleta pamoja kaunti nane za mashariki ya Kenya ambao utatusaidia kutoa mgombeaji mwenye nguvu wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alisema Gavana Mutua. Kulingana na takwimu za IEBC, kuna zaidi ya wapigakura 3 milioni waliosajiliwa katika kaunti hizo nane.

Bw Kiraitu alisikitika kwamba kwa muda mrefu, eneo la mashariki ya Mlima Kenya limechukuliwa kama mgeni katika siasa za nchi tangu uhuru. Gavana huyo wa chama cha Jubilee ametangaza azma ya kuunda chama cha eneo la Mlima Kenya mashariki atakachotumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Gavana Mutua ni kiongozi wa chama chake cha Maendeleo Chap Chap na ametangaza kuwa atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tumechoka kuwa watazamaji na kuchukuliwa kama wageni katika ngoma ya siasa kwa miaka mingi. Wakati huu, eneo la mshariki ya mlima limefungua macho na tuko tayari kuungana na wenzetu kama Mutua, Kalonzo Musyoka (kiongozi wa chama cha Wiper) Charity Ngilu (Narc) na vyama vingine ambavyo vinatetea maslahi yetu ya kisiasa kwa kuwa sasa tunafufua chama chetu,” alisema Bw Kiraitu.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Kiraitu alikuwa akiongoza chama cha Alliance Party of Kenya (APK) ambacho ni moja ya vilivyovunjwa kuunda chama cha Jubilee.

Mnamo Jumatano, Bw Kiraitu alitangaza kuwa Jubilee imekufa kaunti ya Meru na akafichua kuwa ataunda chama cha kisiasa atakachotumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Magavana hao walikuwa wameandamana na wabunge na madiwani kadhaa katika mazishi ya Eunice Karegi aliyekuwa MCA katika bunge la kaunti ya Meru.

Kauli yao inajiri wakati mzozo umezuka kati ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya mashariki na Mlima Kenya magharibi kufuatia kutawazwa kwa Spika wa Bunge Justin Muturi kuwa msemaji wa eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

KDF waua magaidi wawili wa al-Shabab

Wito wazee wa nyumba 10 walipwe kusambaza kadi za Huduma...